Fufa: Uganda malengo yetu ni kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026

Muktasari:

Fufa imetangaza lengo lao la kwanza kwa sasa ni kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026, litakalofanyika Canada, Mexico na Marekani.

Kampala, Uganda. Maisha mipango na malengo ya muda mfupi na mrefu ndiyo siri ya mafanikio.

Unapofanikiwa kuvuka hatua moja ni busara kuweka lengo lingine kubwa katika kupiga hatua nyingine ya maendeleo.

Ndicho walichoamua kufanya Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) baada ya kutangaza mapema lengo lao kubwa kwa sasa ni kufuzu kwa Kombe la Dunia FIFA 2026, litakalofanyika katika nchi tatu za Canada, Mexico na Marekani.

Mpango huyo umekuja baada ya kupata mafanikio katika ule wa kwanza wa kuhakikisha Afcon 2019 wanacheza hatua ya mtoano, huku mwaka 2017, Uganda ilifuzu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 38 kucheza Afcon.

Rais wa Fufa na mjumbe wa mkutano mkuu wa CAF, Moses Magogo aliweka bayana juu ya mpango mpya wa shirikisho hilo.

 “Leo tumefika mwisho wa mpango wetu wa kwenda Cameroon uliozinduliwa Novemba 24, 2014. Ulikuwa ni mpango uliotekelezeka kwa vitendo, uzoefu na mafanikio makubwa.

“Pia leo tunazindua mpango mwingine wa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026. Pia tutahakikisha tunafuzu kwa mashindano yote kuanzia yale ya vijana na wakubwa katika kutimiza lengo letu. Kwa kulitimiza hilo tunataka kufuzu CHAN 2020, 2022, 2024 na 2026, pamoja na AFCON 2021, 2023 na 2025,” alisema Magogo.

Uganda Cranes pia inajiandaa na mashindano Cosafa 2019 ikiwa nchi mwaliko wa mashindano hayo ya kusini mwa Afrika.

Katika mechi ya kwanza ya kusaka kufuzu kwa CHAN 2020, Uganda Cranes itacheza dhidi ya Somalia.