Ufungaji bora England ni vita ya Mo Salah, Kane, Aguero, Aubameyanga

Monday August 6 2018

 

London, England. Mshambuliaji nyota wa Liverpool aliyetwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu England msimu uliopita Mohammed ‘Mo’ Salah raia wa Misri, anatarajiwa kupata ushindani mkubwa katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu.

 

Mo Salah alimpiku Harry Kane wa Tottenham katika mechi za mwisho mwisho katika Ligi Kuu England hivyo kumaliza msimu akiwa amefunga mabao 32 dhidi ya 30 ya Kane katika mechi 38 za Ligi hiyo yakiwa ni mabao mengi katika misimu ya hivi karibuni.

 

Mo Salah (Liverpool)

Mshambuliaji huyo atakuwa na kibarua cha kuhakikisha anatetea tuzo yake akiongoza mashambulizi ya Liverpool msimu huu.

Harry Kane. Tottenham Hotspurs

Hata hivyo kiwango kizuri kilichoonyeshwa na Kane katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia akitupia mabao sita ni wazi kuwa Mo Salah atakuwa na kazi pevu kutwaa tena kiatu cha dhahabu.

Sergio Aguero. Manchester City.

Mbali ya Kane pia atakabiliwa na ushindani kutoka Sergio Aguero, ambaye jana aliifungia Manchester City mabao yote ilipoichapa Chelsea kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii. Mshambuliaji huyo aliibuka mfungaji bora wa Ligi msimu wa 2014-15, alipofunga mabao 21.

Romelu Lukaku. Manchester United.

Mshambuliaji mahiri wa Manchester United, Romelu Lukaku amedhihirisha kuwa alistahili kupewa jezi namba 9, msimu uliopita alifunga mabao 16 na kasi ya ufungaji aliyoionyesha katika fainali za Kombe la Dunia inadhihirisha atakuwa moto wa kuotea mbali msimu huu.

Pierre-Emerick Aubameyang. Arsenal.

Mshambuliaji mahiri kutoka Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang aliyehamishia makali yake Arsenal, akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani Januari mwaka huu kwa ada ya Pauni 56 milioni, alifunga mabao kumi katika mechi 13 aliyoichezea Arsenal chini ya Arsene Wenger na anatarajiwa kumpa mwanzo mzuri Kocha mpya Unai Emery.

 

Advertisement