Uenyeji kufuzu Olimpiki wawapa mzuka wavu Tanzania

Muktasari:

Tanzania imepangwa kundi B na timu za Niger, Ghana, Afrika Kusini na Sudan katika mashindano ya mkondo wa pili na timu zitakazofanya vizuri zitacheza mashindano ya Afrika baadae mwaka huu na mabingwa wataliwakilisha bara hilo kwenye Olimpiki 2020.

Dar es Salaam.Baada ya Shirikisho la mpira wa wavu la Afrika kuipa Tanzania uenyeji wa mashindano ya mkondo wa pili ya kutafuta tiketi ya kufuzu kushiriki Olimpiki, nafasi hiyo imewaibua nyota wa timu ya Taifa ya wavu ya ufukweni.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Wavu (Tava), Fred Selengia yatafanyika Machi 13 hadi 15 kwenye fukwe ya Mbalamwezi, Dar es Salaam.

Timu ya Taifa itaingia kambini Februari 20 kujiandaa na mashindano hayo ambayo Tanzania itawakilishwa na wachezaji wanne.

Wakizungumzia ushiriki wao, wachezaji hao kwa nyakati tofauti walisema wataitumia nafasi ya kuwa mwenyeji kuhakikisha wanafuzu kucheza mashindano ya Afrika na baadae Olimpiki.

Ford Edward mmoja wa wachezaji hao alisema walipambana katika mashindano ya mkondo wa kwanza nchini Uganda na kuwa mabingwa, ndivyo hivyo hivyo watafanya katika mechi za mkondo wa pili.

Mchezaji mwingine, Said Alhaji alisema licha ya ugumu wa mashindano hayo, lakini hawawezi kuwaangusha Watanzania wakicheza nyumbani.

"Lengo letu ni kufuzu kucheza Olimpiki, mpaka sasa ni kama tumetanguliza mguu mmoja ndani, tutapambana kwa nguvu, uwezo na morali ya hali ya juu ili kuhakikisha hatupotezi nafasi hiii.

Wachezaji wengine ambao wako kwenye kikosi cha Taifa ni Shukuru Ally na David Neeke.