Uefa watu wamefokeana

Muktasari:

Mchezo wa kwanza ulikuwa kati ya Barcelona na Napoli ambapo Barca iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kuifurusha nje Napoli kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya mchezo wa kwanza timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

BARCELONA, HISPANIA. MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya imeendelea jana Jumapili ikiwa ni hatua ya 16 bora ambapo michezo miwili ilipigwa na miamba wa soka ambapo Bayern Munich na Barcelona walitinga hatua ya robo fainali ya michuao hiyo.

Wababe wa Hispania, Barcelona walicheza na Napoli ambapo Barca iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kuitupa nje Napoli kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya mchezo wa kwanza timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Bayern Munich iliyokuwa nyumbani ikiialika Chelsea ambapo Bayern iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na  kutinga hatua ya robo fainali kwa jumla wa mabao 7-1, baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa pale London, Bayern kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Baada ya mchezo huo straika wa Bayern Robert Lewandowski aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye michuano hiyo akiwa amefunga jumla ya mabao 66.

Pia kipigo hicho cha 7-1 ilichopokea Chelsea kimeifanya kuwa klabu ya pili kutoka England kuwahi kupokea kipigo kikubwa  nyuma ya Arsenal ambayo ilikubali kichapo cha mabao 10-2 kwa ujumla wa mchezo wa kwanza na wa pili msimu wa 2016/17 dhidi ya hao hao Bayern Munich.

Baada ya hatua hiyo ya 16 bora kumalizika ratiba ya robo fainali imetoka na Atlanta itaumana na PSG Agosti 12 saa 4:00 usiku, RB Leipzig itakipiga dhidi ya Atletico Madrid siku itakayofuata ya Agosti 13 saa 4:00 usiku.

Barcelona itakuwa na kibarua mbele ya Bayern Munich Agosti 14 saa 4:00 usiku, Manchester City itamaliza na Olympique Lyon Agosti 15 saa 4:00 usiku.