VIDEO: Uchaguzi Yanga wasimamishwa

Friday January 11 2019

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imesitisha uchaguzi wa Yanga uliokuwa ufanyike Jumapili ya tarehe 13, 2019, hadi itakapopokea oda ya Mahakama.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ally Mchungahela amesema mchakato wa uchaguzi huo umesitishwa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi katika mikoa ya Dar es Salaam,  Mbeya na Morogoro.
"Tukiwa kwenye kikao cha mwisho cha maandalizi ya uchaguzi,  tulipata taarifa kuhusu baadhi ya kesi kufunguliwa mahakamani kupinga uchaguzi,"alisema Mchungahela.
"Hatutaki kwenda kinyume na mahakama, tumeamua kusitisha mchakato huo hadi tutakapopata oda ya mahakama," alifafanua Mchungahela.
Alisema mchakato wa nini kitaendelea kuhusu uchaguzi huo itajulikana Jumatatu: "Tunaomba wagombea wote wasitishe kampeni kuanzia sasa, "alisema.
Gazeti la Mwanaspoti leo Ijumaa ya Januari 11, liliandika habari kuhusu uchaguzi wa Yanga uko njia panda.

UCHAGUZI YANGA NJIA PANDA
KAMPENI za wagombea wa uongozi katika Uchaguzi Mdogo wa Yanga zimepamba moto, huku wanachama wa klabu hiyo wakiwa bize kuhesabu saa kabla haujafanyika Jumapili, lakini ghafla tu upepo umebadilika.
Inaelezwa kuwa uchaguzi huo upo njia panda kufanyika, baada ya baadhi ya wanachama kujipanga kukimbilia mahakamani leo Ijumaa, ili kuuzuia kwa madaia ya kukiukwa kwa katiba yao na namna mchakato mzima ulivyoitishwa hadi sasa.
Lakini wakati wanachama hao wakijipanga hivyo, taarifa zilizonaswa mapema jana zilidokeza kufanyika kwa kikao kizito kwenye Uwanja wa Taifa, kilichohusisha vigogo wa serikali na wale wanaousimamia uchaguzi huo ili kuujadili kwa kina.
Chanzo chetu kilichokuwa Uwanja wa Taifa, kilidokeza kuwa Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka (TFF), Ally Mchungahelo walikutana na viongozi wa serikali kwa muda uwanjani hapo.
Viongozi wanaotajwa kushiriki kikao hicho kizito ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo (BMT) Alex Mkenyenge na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Inaelezwa kuwa mbali na mambo mengine, ishu ya uchaguzi huo wa Yanga ambao umekuwa ukiwekewa mizengwe na wanachama na viongozi wa klabu hiyo tangu ulipotangazwa mwishoni mwa mwaka jana, ilijadiliwa.
Yanga wamekuwa wakiupinga uchaguzi huo kwa sababu ya nafasi ya Uenyekiti kuwekwa katika kinyang’anyiro, huku wenyewe wakiendelea kumtambua Yusuf Manji, ambaye alishatangaza kurejea klabu hapa Januari 15, mwaka huu.
Pia, walikuwa wakipinga TFF na Kamati yake ya Uchaguzi kuusimamia ilihali wakitaka uwe chini ya mamlaka ya klabu kulingana na katiba yao.

ISHU YA KORTINI
Baadhi ya wanachama wa Yanga wamepanga kwenda kuweka zuio mahakamani leo Ijumaa ili uchaguzi huo wa kuziba nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wake sambamba na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji, usifanyike Jumapili.
Wanachama hao wakitumia kampuni ya uwakili ya Taslima Law Chambers Advocates wameibuka na kupinga mchakato wa uchaguzi huo kutumia katiba ya 2010 ambayo wanadai ni batili huku wakidai inayotambulika ni ile ya 1968.
Mwaka 2010 kulikuwa na mkanganyiko wa katiba ipi Yanga iitumie kati ya ile ya 1968, 1992 na 2008 ambazo ziliwahi kutengenezwa kwa ajili ya klabu hiyo.
Kingwaba A. Kingwaba, Juma M.Matimbwa na Siwema Chiokota walifungua shauri la madai namba 98 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakidai kuwepo na mkanganyiko kuhusu katiba rasmi ya kufuatwa kati ya ile ya 1968, 1992 na ya 2008.
Wakili wa wanachama hao, Twaha Taslima alisema katika shauri hilo, katiba ya 1968 ndio ilitajwa na mahakama kuwa halali kuongoza shughuli za Yanga kwa vile inatambulika na zile nyingine haziko kisheria.
“Kwa maana hiyo sasa tunatoa angalizo kwamba, hata uchaguzi wa Januari 13, 2019 ni batili kwani unakiuka amri halali ya mahakama,” alisema wakili huyo na kufafanua kuwa baada ya maamuzi hayo, hakuna usajili uliofanywa wa katiba ya Yanga zaidi ya ile ya 1968 kuendelea.
“Wateja wetu (Kingwaba, Matimbwa na Siwema) wametutaka tuikumbushe TFF suala hili kabla hawajachukua hatua za kisheria kwa yale tunayoyaona yanayoendelea kinyume na katiba tajwa ya Yanga ya 1968,” alisema.
Mwanasheria huyo alisema wanachokitaka ni TFF kutekeleza amri hiyo ya mahakama ndani ya siku mbili tangu siku waliyopata barua ya zuio hilo (yaani juzi Jumatano) katika uchaguzi huo, huku nakala ikipelekwa klabu ya Yanga na Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

WASIKIE

MABOSI SASA
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alikiri kupokea nakala kutoka kwa kampuni hiyo ya sheria, ila alisisitiza Yanga haiwezi kuzungumzia chochote kuhusu uchaguzi huo kwa kuwa unasimamiwa na TFF hivyo, waulizwe TFF wenyewe.
Mmoja wa maofisa wa DRFA ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, pia alikiri kupokea nakala ya barua hiyo kutoka Taslima Law Chambers Advocates lakini, akasisitiza uchaguzi hauko chini yao, hivyo hawezi kusema chochote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Ally Mchangahela alipoulizwa alisema hajapata taarifa hizo na atakwenda kufuatilia kwa undani TFF ili kujua ukweli ukoje kuhusiana na hilo.
Ingawa Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Ibrahim Mkwawa alisema Katiba ya Yanga ambayo Baraza la Michezo la Taifa (BMT) inaitambua ni ile ya 2010.
“Hao wanaotaka kuturudisha kwenye Katiba ya 1968 hiyo imepitwa na wakati, inayotambulika ni ile ya 2010 ambayo iko Baraza na ndio itatumika kwenye uchaguzi wa Jumapili ambao ni maalumu kuziba nafasi zilizo wazi ambayo ni ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga 2010, Imani Madega alisema hawezi kuzungumzia shauri la wanachama hao na kile kinachoendelea sasa kuhusu uchaguzi wa Yanga kwa kuwa, alishatoka kwenye masuala ya soka.
“Sipo kabisa kwenye masuala ya soka, hivyo siwezi kuzungumzia chochote kuhusu hao wanachama wala uchaguzi wa Yanga, kwanza sijui chochote kinachoendelea huko, niko shambani nalima,” alisema Madega.


ISHU YA KIKAO
Mwanaspoti ilimtafuta Katibu Mkuu wa BMT, Alex Mkenyenge ambaye alipoulizwa juu ya taarifa ya kukutana faragha na kudai hakuna kitu kama hicho, lakini Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo alipoulizwa akikiri ni kweli walikuwa kwenye kikao na wanajadili mambo mengi, lakini ishu ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa Yanga, alidai hakuna na kuwa kikao chao bado kilikuwa bado kinaendelea.


MANJI ATAJWA
Katika hatua nyingine baadhi ya wanachama wa Yanga wamesisitiza wanamsubiri kwa hamu Manji atimbe klabuni kwao kama alivyowaahidi kwenye barua aliyoiandikia Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.
Kwenye barua hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, George Mkuchika ilieleza kuwa Januari 15, mwaka huu, Manji ataanza kazi rasmi klabuni kwani tatizo lake la kiafya lilitarajiwa kumalizika Desemba 15, mwaka jana kwa mujibu wa madaktari wake.
Hata hivyo, serikali ilishasisitiza kuwa, Manji sio Mwenyekiti wa Yanga baada ya kutangaza kujiuzulu Mei 20, 2017 na kushindwa kuonekana klabu kwa muda mrefu licha ya wanachama kusisitiza wanamtambua.
Wanachama hao walirejea barua ya Julai 11, 2018 ya TFF kwenda kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wao, Clement Sanga iliyomuengua kwenye Bodi ya Ligi (TPLB) kama Mwenyekiti kwa vile ilikuwa ikimtambua Manji kama Mwenyekiti wa Yanga.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea wagombea mbalimbali wanaowania nafasi za uongozi ndani ya Yanga, kwa sasa wanaendelea na kampeni zao zilizoanza mapema wiki hii ili kujaribu kushawishi wanachama kuwapigia kura kwenye uchaguzi huo wa Jumapili.

Advertisement