Uchaguzi Yanga wamng'oa kigogo

Saturday December 8 2018

 

By KHATIMU NAHEKA

UCHAGUZI wa Yanga unaendelea kukumbwa na vitimbi vya kila kukicha, ambapo baada ya juzi Mjumbe wa klabu hiyo Daniel Mlelwa kuitaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kutaka mchakato wa uchaguzi huo kurudiwa upya, mambo zaidi yamezidi kutikisa.
Juzi, Mlelwa aliitaka Kamati hiyo ya TFF inayoongozwa na Ally Mchangahela kuahirisha mchakato wa usajili kwa wagombea kwa kuwa, kuendelea ni kukiuka Katiba ya Yanga, lakini akawekewa ngumu na kuamua kususia kushiriki kwenye uhakiki huo, kigogo muhimu ndani ya wababe hao wa Jangwani, ametangaza kujiengua kwenye uchaguzi huo.
Kigogo huyo Hamad Islam, ambaye ni miongoni mwa watu muhimu ndani ya Yanga wanaojitoa kwa hali na mali kusaidia kikosi hicho kufanya kweli, amesema amelazimika kujiondoa baada ya kutakiwa kufanya hivyo na familia yake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Islam ambaye amekuwa nguzo muhimu kwa Yanga hasa inapoweka kambi mkoani Morogoro, amesema familia yake imemtaka kuachana na uchaguzi huo.
Alisema ameamua kuchukua maamuzi hayo baada ya mama yake mzazi kumtaka kuachana na uchaguzi huo na kushindwa kupingana na mzazi wake huyo.
"Nimeona nichukue uamuzi huo wa kukubaliana na familia yangu, naona shinikizo limekuwa kubwa kila unachofanya ni lazima upate baraka za familia," alisema Islam.
"Nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu wa Yanga, lakini kwa sasa sitaweza kuendelea na nia ya kuendelea na uchaguzi."

Advertisement