Ubingwa wa Simba watua bungeni, wengine wapinga

Wednesday May 22 2019

 

By Ibrahim Yamola

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameipongeza Klabu ya Simba kwa kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara 2018/19.

Simba jana Jumanne ilitawazwa mabingwa baada ya kuichapa Singida United kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nafua mkoani Singida.

Leo Jumatano Mei 22, 2019 mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Spika Ndugai alitoa matangazo ikiwamo la Simba kutetea ubingwa wa 20 akisema, “wale wanaoutafuta ubingwa waendelee.”

Kauli hiyo iliwafanya wabunge kushangilia huku sauti ikisikika ikitoka ‘wa mbeleko ya chuma’ na nyingine ‘ubingwa wa TFF.’

“Tunawapongeza Simba kwa kuibuka mabingwa, hongereni sana Simba. Hongereni sana Yanga kwa juhudi za kuongoza ligi kwa muda mrefu,” amesema Spika Ndugai ambaye pia ni shabiki wa Simba

Pia, kiongozi huyo wa Bunge, amempongeza Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa kupandisha timu ya jimboni kwake ya Namungo itakayoshiriki Ligi Kuu msimu ujao wa 2019/20.

Advertisement

Ametoa wito kwa wabunge wengine kuiga mfano huo kwa kuhakikisha inazipandisha timu za majimboni mwao kwani michezo inakuza utaifa.

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai ametoa wito kwa wabunge wanaotaka kwenda Misri kushuhudia michuano ya Fainali ya Afcon kuhakikisha wanajiandikisha mapema iwezekanavyo ili kutokosa hoteli.

Advertisement