Ubingwa Simba uko hapa

Muktasari:

Mechi hizo tano za viporo ambazo zinaiweka Simba matatani ama ndio zinaweza kuamua hatima ya ubingwa wake ni dhidi ya timu za Azam, Prisons, Kagera Sugar, Lipuli pamoja na Mtibwa Sugar ambazo ziko mbele yake.

USHINDI wa bao 1-0 dhidi ya Yanga umewapa jeuri mashabiki wa Simba ambao, wanaamini njia ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ni nyeupe kwao licha ya viporo nane walivyonavyo mkononi.

Licha ya kuachwa kwa tofauti ya pointi 19 na Yanga inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 58, Simba ina faida kutokana na kucheza mechi nane ambazo ni viporo vilivyotokana na ushiriki wake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ushindi kwenye mechi hizo nane za viporo utaifanya Simba kuzoa jumla ya pointi 24 ambazo ukichanganya na 39 ilizonazo sasa, itafikisha 63 ambazo zitaifanya iipiku Yanga kwa tofauti ya pointi tano huku wakiwa na idadi sawa ya mechi.

Hata hivyo, wakati Simba wakipigia hesabu mechi zao nane za viporo huku wakizitazama kama silaha yao ya kuwapiku Yanga, kuna mechi tano za kibabe katika viporo hivyo ambazo zinaweza kuvuruga mipango yao ya kutetea ubingwa.

Mechi hizo tano za viporo ambazo zinaiweka Simba matatani ama ndio zinaweza kuamua hatima ya ubingwa wake ni dhidi ya timu za Azam, Prisons, Kagera Sugar, Lipuli pamoja na Mtibwa Sugar ambazo ziko mbele yake.

Ushindani wa timu hizo dhidi ya vigogo wa soka nchini ni mkubwa huku rekodi zikionyesha si nzuri kwa Simba pindi inapokabiliana nazo pamoja na historia ya ugumu kwenye viwanja ambavyo mechi hizo zitachezwa, vinafanya mechi hizo kuwa mlima mrefu kwa mabingwa hawa watetezi.

Mechi dhidi ya Azam FC inatabiriwa kuwa na upinzani wa aina yake kutokana nafasi za timu hizo mbili katika msimamo wa ligi.

Azam iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 49, iwapo ikiruhusu kufungwa maana yake itaandaa mazingira ya kuachwa kwa idadi kubwa ya pointi na Simba ikiwa baadaye itapata ushindi kwenye mechi zake za viporo.

Lakini, Azam FC ina kundi kubwa la wachezaji wazoefu wanaoifahamu vyema Simba wakichagizwa na uwepo wa benchi imara la ufundi chini ya Hans Pluijm, ambaye ameifunga Simba mara nne tangu alipoanza kufundisha soka nchini.

Pia, Simba ina kibarua kizito ugenini mbele ya Kagera Sugar, Lipuli na Prisons ambako imekuwa haina rekodi ya kufanya vyema katika viwanja vitakavyochezwa mechi hizo.

Timu hizo zimekuwa na historia tamu ya kuleta upinzani na kuchukua pointi mbele ya Simba pindi zinapokuwa nyumbani, lakini hata zinapocheza ugenini.

Ukiondoa msimu uliopita, kwenye misimu mitano iliyopita, Simba haikuwahi kuzoa pointi zote dhidi ya timu za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine huku Prisons ikiwatibulia mara kwa mara zinapokutana.

Lakini, kama hiyo haitoshi, Simba wana mechi dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, ambako wamekuwa wakiangusha pointi mara kwa mara huku pia wakikabiliwa na jinamizi la kupoteza pointi kila msimu pindi wanapocheza Kanda ya Ziwa.

Katika kulidhihirisha hilo, tayari wameshaangusha pointi pindi walipofungwa bao 1-0 na Mbao FC katika mzunguko wa kwanza jijini Mwanza.

Kibarua kingine ni dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, ambapo Simba wataingia wakiwa hawana rekodi ya kuifunga timu hiyo tangu ilipopanda Ligi Kuu msimu wa 2017/2018.

Katika mechi tatu ambazo timu hizo zimekutana tangu Lipuli walipopanda daraja, zimetoka sare mara zote.

Ukiondoa mechi hizo, Simba pia watakuwa na mtihani mbele ya Mtibwa Sugar nyumbani. Msimu uliopita, Mtibwa iliisimamisha Simba hapa jijini kwa kutoka nayo sare ya bao 1-1 lakini msimu huu tayari imewachapa Azam FC kwa mabao 2-0 katika mchezo uliozikutanisha mkoani Morogoro wiki tatu zilizopita.