UTATU: Ukikutanao utaokota mipira nyavuni hadi uchoke

Muktasari:

Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League itashuhudia mechi zake za mwisho za kukamilisha hatua ya makundi na baada ya hapo itasimama hadi Februari mwakani ndipo itakapoanza rasmi hatua ya mtoano.

HAWA watu ukikutana nao watakutekenya utacheka tu. Hata kama ni mpinzani wao, itakubidi ukubali tu na hali halisi.
Desemba ndio hiyo imefika na kuna ligi kadhaa za Ulaya ukiondoa ile ya Ligi Kuu England zitasimama ndani ya mwezi huu kupisha baridi na Sikukuu ya Krismasi.  England wao hawana hizo, kitu kinaendelea kupigwa tu haina kuremba.
Kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League itashuhudia mechi zake za mwisho za kukamilisha hatua ya makundi na baada ya hapo itasimama hadi Februari mwakani ndipo itakapoanza rasmi hatua ya mtoano.
Lakini kwa sasa makala haya yanahusu safu tano matata zinazoundwa na washambuliaji watatu ambazo zinatamba kwenye Ligi Kuu za Ulaya kwa msimu huu wa 2018/19 hadi kufikia sasa.

5.Sterling, Aguero & Sane- mabao 22
Manchester City imekuwa timu ngumu sana kuizuia kwa mwaka wa pili mfululizo kwenye Ligi Kuu England kutokana na kile ilichokifanya hadi sasa. Kikosi hicho cha Etihad kinachofahamika kwa jina la utani la The Citizens bado hakijapoteza mechi yoyote ya ligi hadi sasa, huku Liverpool pekee ndiyo inaofanana nayo kwenye rekodi hiyo kwa msimu huu. Kocha wake, Pep Guardiola amefanya kazi nzuri ya kutumia pesa kufanya usajili wa akili tofauti na mpinzani wake, Jose Mourinho ambaye amesajili bila ya kutumia akili.
Pep ametengeneza safu yake ya ushambuliaji ya mastaa watatu inayoundwa na Raheem Sterling, Sergio Aguero na Leroy Sane, ambao kwa pamoja imehusika kwenye mabao 22.
Aguero na Sterling kila mmoja amefunga mabao manane, wakati Sane amefunga sita.

4.Messi, Suarez & Dembele- mabao 23
Uamuzi wa Neymar kuachana na Barcelona na kutimkia PSG mwaka 2017 ulifungua milango ya mshambuliaji mwingine kutua Nou Camp kwenye kuziba pengo lake kwenye kikosi hicho. Barcelona iliamua kuwasajili Ousmane Dembele na Philippe Coutinho kujaribu kuziba pengo hilo lililoachwa na Mbrazili huyo. Wawili hao, Dembele na Coutinho wanafanya vizuri, lakini kinda wa Kifaransa ndiye aliyepewa majukumu ya kucheza  kwenye eneo la ushambuliaji zaidi kuziba pengo hilo la Neymar.
Msimu huu, Dembele amefunga mabao matano, lakini muda mwingi akiwa anatokea kwenye benchi.
Supastaa Lionel Messi amefunga mabao tisa kama ilivyo kwa mshambuliaji mwenzake Luis Suarez, ambaye amefunga mabao tisa pia na kufanya watatu hao wa Barcelona kufunga mabao 23.

3.Paco, Reus & Sancho- mabao 23
Borussia Dortmund kwa namna ilivyoanza kwa kasi msimu huu kwenye Bundesliga umewasapraizi wengi sana. Hilo limewashtua watu kwa sababu wanajiuliza mabao yanatokea wapi tena baada ya kumuuza Aubameyang kwenda Arsenal kwenye dirisha la uhamisho wa Januari mwaka huu.
Lakini jeshi hilo linalotumia jezi za rangi ya manjano na nyeusi limekuwa kali kweli kweli na kuangusha tu vichapo kwenye ligi hiyo msimu huu.
Si tu inaoongoza ligi ikiwa na pointi 33, lakini imecheza mechi 13 bila ya kupoteza mchezo wowote hadi sasa.
Kuna sababu kadhaa zinazoifanya Borussia Dortmund kuwa tishio kwa msimu huu na moja ya makali yake na ni ile safu yao matata kabisa ya ushambuliaji inayoundwa na wakali watatu ambao wamekuwa tishio kwa mabeki. Washambuliaji hao ni Paco Alcacer, aliyefunga mara 10, huku mabao yake mengi akitokea benchi, huku Marco Reus yupo vizuri akifunga mara tisa na Jadon Sancho amefunga mara nne kuwafanya kuwa na jumla ya mabao 23.

2.Jovic, Haller & Rebic- mabao 24
Eintracht Frankfurt wanafurahia mwanzo wao mzuri kwenye Bundesliga hadi sasa msimu huu. Makali yao yamenogeshwa zaidi na safu yake ya washambuliaji watatu ambao wamekuwa wakisababisha matatizo makubwa kwa mabeki wa timu pinzani.
Kwa ujumla wake, safu hiyo ya washambuliaji watatu inaundwa na Luka Jovic, Sebastien Haller na Ante Rebic, ambao kwa pamoja imefunga mabao 24.
Kwa mgawanyiko wao wa mabao, Jovic amefunga mabao 10, wakati Haller amefunga tisa na Rebic amefunga mabao matano na kufanya safu yao kuwa tishio kwa wa timu kadhaa kwenye Bundesliga msimu huu. Timu hiyo kwa kwa sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 23, ikishuka uwanjani mara 13 ikishinda mara saba, sare mbili na vichapo vinne.
Kwa jumla wa kikosi kizima kimefunga mabao 30, hii ina maana wachezaji wengine wasiokuwa Jovic, Haller na Rebic wamehusika kwenye mabao sita tu.

1.Mbappe, Neymar & Cavani- mabao 33
Mabingwa watetezi wa Ligue 1 na vinara wa ligi hiyo kwa msimu huu Paris Saint-Germain Jumatano iliyopita waliduwazwa baada ya kutoka sare ya 1-1 na Strasbourg.
Yalikuwa matokeo yaliyowashangaza wengi, lakini hivyo ndivyo soka ilivyo na upekee wake. Hata hivyo, sare hiyo bado inawafanya waendelee kutamba kwenye ligi hiyo, wakiongoza kileleni kwa tofauti ya pointi 14. Kwenye sare hiyo, Edinson Cavani ndiye aliyefunga bao kupata sare. Lakini jambo kubwa linaloifanya PSG kuwa tishio ni safu yake ya washambuliaji watatu kuwa na kasi ya kutisha kwenye kufunga mabao.
Ukweli ni kwamba akikosa Cavani basi Kylian Mbappe na mwenzake Neymar watakufunga. Wakali hao wote wapo vizuri kwenye kupasia mipira nyavuni na ndio maana kwa pamoja wamehusika kwenye mabao 33, Mbappe akiwa kinara akifunga 12, anafuatiwa na Neymar mwenye mabao 11 na Cavani akifunga mara 10. Hiyo ndiyo safu inayoundwa na washambuliaji watatu hatari zaidi huko kwenye ligi za Ulaya kwa sasa.