UCHAMBUZI: Ubunifu na fikra mpya zinahitajika katika soka

WAKATI mwaka 2020 ukikaribia kumalizika ili kuukaribisha 2021 katika soka ni vema tukawa na utaratibu wa kuangalia tulipotoka, huku tukipanga kwenda tunakotarajia kufika siku zijazo.

Hii ni kawaida tu kwani hata waswahili wanasema ili ujue unakokwenda ni lazima kwanza ujue ulipotoka.

Katika soka nchini ukiangalia tulipotoka kisha ukaangalia tunapoelekea unaweza kuuona mwanga au dalili zake kwa kiasi fulani, hasa baada ya dunia ya sasa kuwa wazi na kufunguka kwa kila kitu kinachofanyika katika mataifa mbalimbali duniani.

Katika soka kuweza kuonekana moja kwa moja kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano. Ingawa katika mchezo wa soka mafanikio hupimwa kwa idadi ya vikombe vya ushindi, lakini kuelekea kwenye kutwaa huo ushindi au mataji huwa kuna njia ndefu ambayo kila mshindani hutakiwa kuipita.

Ndio maana nasema tunaweza kuna mwanga kwa kuwa bado tupo njiani na watanzania walikwishathibitika kuwa na mapenzi ya dhati na mchezo wa soka.

Kuelekea katika maendeleo yoyote huwa kuna changamoto nyingi ambazo huhitaji ubunifu ili kuweza kuzitatua changamoto hizo, kwani bila ya kubuni vitu vipya maana yake itakuwa ni sawa na kurudia yaleyale.

Hivyo kuendelea na mawazo na fikra za nyakazi za mani wakati kila zama huja na mambo tofauti kama ilivyokuwa zamani ilikuwa soka la ridhaa kwa sasa ni soka la kulipwa, hivyo tofauti hiyo ni kubwa sana inayohitaji ubunifu na weledi wa kiwango cha juu katika kutekeleza majukumu ya uendeshaji wa soka.

Kwa mfano Afrika wiki iliyopita tulishuhudia mechi za nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zikichezwa ambapo timu nne kutoka katika mataifa mawili ya Morocco na Misri ndizo zilifanikiwa kufika katika hatua hiyo.

Hivyo kuendelea kutoa uhakika wa bingwa wa msimu wa 2019/2020 wa mashindano hayo pia kutoka katika nchi za Ukanda wa Afrika Kaskazini, huku timu za Misri, Al Ahly na Zamalek zikishinda mechi za kwanza.

Ukiangalia kile ambacho mataifa yaliyopo katika katika ukanda huo wa Afrika Kaskazini utaona kuwa, wanachokifanya ni kama kile nilichoanza kusema huko mbele wanaangalia historia ya kule walipotoka na kuona namna ambavyo wazee wao waliotangulia walivyofanikiwa kufanya vizuri miaka hiyo.

Hivyo na wao kuja na mawazo na fikra mpya za kuhakikisha kwanza wanavunja rekodi zote za mafanikio yaliyopatikana miaka ya nyuma kisha wanaweka mpya, hivyo kusababisha kila kizazi kuwa na utashi wa kutaka kuweka rekodi mpya ya mafaniko ndio maana mataifa hayo yamekuwa yakiendelea kufanikiwa kila uchao katika nafasi ya klabu Afrika.

Mawazo mapya na fikra mpya ni kitu ambacho nasi pia katika soka la Tanzania tunatakiwa kukifanyia kazi kwenye soka letu, kwani wote hao tunaowataja tunasema wanaendelea katika tasnia hii ya soka ni kwa vile pamoja na kuangalia historia, lakini siku zote wanaonekana kuwa na mawazo mapya kila kukicha hivyo kuwafanya waendelee kukaa katika eneo la mafanikio.

Kwani ya mawazo na fikra mpya klabu mbalimbali vya sioka katika mataifa ya Morocco, Misri, Algeria na Tunisia visingeweza kuwa na uwezo wa kulipa mishahara wachezaji inayofanana na ile ya wachezaji wanaocheza katika ligi kubwa Ulaya.

Mfano mwingine wa fikra na mawazo mapya ni kama vile tumeshuhudia mwaka huu moja kati ya timu kubwa kabisa England ya Manchester United ikifungua kituo kikubwa cha kuonesha mechi zake Beijing, China ambapo mawazo hayo yalikuwepo tangu mwaka jana ambapo viongozi wa timu hiyo walipanga kufungua vituo vya mashabiki wa timu hiyo katika miji mitatu ya China.

Kumbuka timu ya Manchester United katika kipindi cha Covid-19 ilipoteza kiasi cha Dola 130 milioni kwa mashabiki kutokuruhusiwa kuingia viwanjani katika mechi za ligi.

Hivyo uwepo wa kituo hicho nchini China utawarejesha mashabiki kufuatilia mechi za timu yao wanayopenda kupitia kituo hicho.

Njia hiyo ya kufungua vituo vya China ni moja katika ya mawazo mapya ambayo yametokana na changamoto waliyokutana nayo ya janga la corona, lililosababisha klabu nyingi kuyumba kiuchumi, hivyo kuhitaji vyanzo vipya vya mapato yatokayo kwa wapenzi na mashabiki wa timu husika. Kwa hapa Bongo pia tunatakiwa kuwa na mawazo na fikra kama tunavyoona wenzetu wanavyofanya na sio lazima fikra hizo na mawazo hayo yawe sawasawa na mawazo na fikra zao kwnai tunatofautiana katika maeneo mengi kuanzia utamaduni, uelewa, uchumi na hadi teknolojia, hivyo furaha ya huku inaweza kuwa tofauti na furaha ya sehemu nyingine duniani.