UCHAMBUZI: Soka letu linapenda zaidi utovu wa nidhamu

KUNA matukio mengi ambayo yamekuwa yakitokea katika mechi za Ligi Kuu Bara ambapo yapo yanayoudhi na kuna yanayofurahisha.

Miongoni mwa mambo yasiyofurahisha katika Ligi Kuu ni rafu za kijinga na za makusudi ambazo wachezaji wamekuwa wakifanyanya lakini pia vitendo vya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wachezaji.

Ni matukio yaliyoanza zamani na ilitegemewa kuwa baada ya mechi za Ligi Kuu Bara kuanza kuonyeshwa katika luninga, yangepungua kwa kiasi kikubwa lakini kinyume chake yameonekana kuongezeka.

Nidhamu za wachezaji wengi katika nyakati hizi zimekuwa chini katika hali inayoogopesha na wengi wao hawaonyeshi wasiwasi wa wanayoyafanya ndani ya uwanja ambayo ama yanaweza kupelekea waonyeshwe kadi nyekundu ama kupewa adhabu za kufungiwa na faini ya fedha.

Wengi wanajiuliza kwa nini matukio haya yanazidi kuongezeka kadri siku zinavyosogea badala ya kupungua? Zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea kuota mizizi kwa tatizo la utovu wa nidhamu na rafu mbaya ambazo wachezaji wetu wa timu mbalimbali wamekuwa wakiendelea kufanya kila kukicha.

Kati ya hizo, mbili zinaweza kuwa chanzo cha kuendelea kujirudia na kushamiri kwa matukio hayo ambazo ni makosa ya waamuzi wetu kutotoa adhabu stahiki kwa wachezaji wanaoyafanya lakini sababu ya pili ni udhaifu wa mamlaka za soka kutochukua kwa wakati hatua stahiki kwa wale wahusika wa vitendo hivyo.

Waamuzi wetu wamekuwa wakilea matukio ya utovu wa nidhamu na rafu za mara kwa mara kwa kutowaonyesha kadi wachezaji wengi ambao wamekuwa wakifanya hivyo katika mechi mbalimbali.

Wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa kuhofia lawama za kuonekana wanapendelea upande mmoja ama kuharibu ladha ya ushindani wa mechi kwa kutoa kadi na faulo za mara kwa mara katika mchezo husika.

Lakini kwa upande wa mamlaka zenyewe, zimekuwa zikichukua muda mrefu kutoa uamuzi dhidi ya wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi, waamuzi na hata viongozi wa timu ambao wamekuwa wakijihusisha na utovu wa nidhamu na wakati mwingine kutowapa adhabu kabisa.

Na hata pale zinapochukua hatua, mara nyingi uamuzi umeonekana kuzipendelea zinazoitwa timu kubwa nchini kwa ama kwa wachezaji wao kupewa adhabu nyepesi ama kutoadhibiwa moja kwa moja huku wale wa timu nyingine wakikutana na adhabu kali za vifungo na faini za fedha.

Matokeo ya hili ni kujenga roho za chuki, vinyongo na visasi kwa wachezaji pindi wakutanapo na kupelekea kufanyiana rafu na vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo vinatia doa mchezo wa soka hapa nchini.

Na kama haitoshi, kutochukuliwa hatua kwa matendo ya utovu wa nidhamu huwafanya watu wajenge mazoea na kuhisi kuwa wanachokifanya ni sahihi na hawawezi kuadhibiwa ama na waamuzi au kamati zinazohusika na usimamizi wa ligi na mashindano mbalimbali.

Yako matukio mengi ambayo yanaweza kuwa uthibitisho tosha wa jinsi gani soka letu limekuwa likiwaendekeza wachezaji watovu wa nidhamu na kushawishi waendelee kurudia makosa yao mara kwa mara.

Mwaka 2015, mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma alimpiga kichwa hadharani aliyekuwa beki wa Simba, Hassan Kessy lakini katika hali ya kushangaza, Ngoma hakuonyeshwa kadi nyekundu wala kupewa adhabu yoyote hadi alipoondoka nchini mwaka huu.

Msimu uliopita tu, beki wa kati wa Simba, Pascal Wawa alionekana kumkanyaga kwa makusudi mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi kama ilivyo kwa kiungo Clatous Chama ambaye alifanya kitendo kama hicho kwa Feisal Salum lakini hakuna hata mmoja kati ya hao ambaye aliadhibiwa.

Ni kama ilivyokuwa kwa beki wa Yanga, Lamine Moro ambaye licha ya kuonekana akifanya kosa la kumpiga teke la shingoni mchezaji wa Mbeya City katika mechi baina ya timu hizo, hakuna adhabu ya aina yoyote ambayo beki huyo raia wa Ghana alipewa ama na refa au mamlaka za soka.

Kuna utitiri wa makosa ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara pasipo kuchukuliwa hatua yoyote na pengine ukurasa huu unaweza usitoshe ikiwa tukiamua kuyaorodhesha na kuyaelezea.

Tunapoamua kuyamazia ama kuwa wazito kuyatolea uamuzi, tunajiumiza wenyewe kwani tunawafanya wachezaji wetu wadhani kuwa wanayoyafanya ni sahihi na hawawezi kuchukuliwa hatua. Matokeo yake wanakwenda kuyafanya hayo katika mashindano ya kimataifa ambayo wanakutana na waamuzi ama mamlaka zisizosita kuwachukulia hatua.