UCHAMBUZI: Prisons ilimchelewesha Stam kuondoka Mbeya City

Thursday October 22 2020
uchambuzi pic

NDOA kati ya Mbeya City na kocha Amri Said ‘Stam’ ilipaswa ivunjike muda mrefu tu, lakini mechi yao na Prisons ambayo walitoka sare tasa ndiyo ilifanya kocha huyo adumu hadi juzi alipovunjiwa mkataba wake.

Mkataba wa Stam na Mbeya City ulikuwa wazi kwamba akiongoza mechi tano bila ushindi, basi unapaswa kuvunjika vinginevyo kungekuwa na makubaliano mengine ambayo pia yasingekuwa rafiki kwa kocha huyo.

Baada ya sare hiyo uongozi wa Mbeya City ni kama ulimvumilia tu kwa kumpa muda huku wakiendelea kutafakari namna ya kupata mbadala wake, lakini ukweli ni kwamba wasingedumu naye hata kwa mzunguko huu wa kwanza.

Ni wazi kwamba sare ya Prisons ilitokana na mechi hiyo kwa Jiji la Mbeya ni kama ‘derby’, hivyo kila upande ulilazimika kupambana angalau kupata matokeo hayo, vinginevyo Mbeya City ingepoteza na ungekuwa ndio mwisho wa Stam na asingesubiri hadi kipigo dhidi ya Mwadui FC cha bao 2-1.

Stam ameiongoza Mbeya City tangu msimu uliopita ambapo pia aliingia katikati wakati timu hiyo ikiwa katika hali mbaya ingawa alifanikiwa kuinusuru isishuke daraja baada ya kucheza mechi za mchujo.

Baada ya ligi kumalizika aliingia kwenye mkataba mpya na timu hiyo - mkataba wenye masharti magumu, lakini alijiamini kwamba angeweza kuipambania timu hiyo ambayo hata usajili wao sio wa ushindani kwa ligi hii yenye ushindani mkubwa.

Advertisement

Stam ni kama alijitega mwenyewe kuongeza mkataba kwenye timu ambayo haijasajili vyema na pengine hata yeye kushiriki katika usajili huo ambao umempa matokeo mabovu tofauti na ilivyotegemewa na wengi kwamba huenda msimu huu Mbeya City ingebadilika na kupata matokeo mazuri.

Mbeya City wameachana na Stam kwa makubaliano ambayo yalikuwepo toka mwanzo kabisa kabla hata ligi haijaanza na sasa ilikuwa ni utekelezaji tu baada ya kushindwa kufikia malengo lakini je kocha atakayekwenda kuifundisha Mbeya City hii atachomokea wapi?

Kikosi cha Mbeya City si kikosi cha ushindani bado kocha atakuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo yale yanayohitajika na viongozi wa Mbeya, pamoja na mashabiki wao labda tu ataponea wakati wa dirisha dogo kama uongozi utaamua kuingia sokoni kusajili wachezaji wenye viwango vya juu.

Kuondoka kwa Stam huenda kukawa pamoja na kuondoka kwa msaidizi wake ambaye ndiye aliyempendekeza.

Na sasa Uongozi wa Mbeya City utakuwa na kazi ya kusaka kocha mkuu ingawa kwao kumpata msaidizi si kazi ngumu kwani tayari yupo Mohamed Kijuso ambaye anafundisha timu ya vijana na amewahi kuwa msaidizi wa timu hiyo ya wakubwa.

Hivyo kwasasa huenda wakati wanasaka kocha mkuu basi Kijuso atarudi tena kuisimamia timu ya wakubwa kuelekea mechi zijazo za Mbeya City ingawa atahitaji nguvu ya ziada kuhakikisha anapambana na kushinda japo kufufua matumaini.

Mbeya City ya sasa imepoteza matumaini, mashabiki huenda pia nao wamekata tamaa kutokana na mwenendo wa timu yao, wana maumivu makali pengine hata mioyo yao inavuja damu.

Lakini, hata hivyo hawana namna kwani tayari ligi imeanza hawana cha kubadilisha na hata kama watabadilisha wakati wa dirisha dogo uongozi uamue kufanya maamuzi magumu ya kutoa fungu la maana na kupata wachezaji bora.

Siioni Mbeya City ambayo inaweza kumaliza ligi kwenye nafasi bora za juu, haipo kabisa mashaka yangu ninayoyaona ni kuiona Mbeya City ile iliyoponea kwenye tundu la sindano ikipotea kabisa kwenye Ligi Kuu ama ikienda tena kwenye mchujo ikafie huko ama kunusurika.

Kikubwa tu ni kwamba uongozi wa Mbeya City utambue kwamba umebeba matumaini makubwa ya Wanambeya ambao ni mashabiki wa timu hiyo.

Hivyo ni vyema viongozi hao wakafanya uamuzi mgumu wa kujitoa kwa kila hali ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inaondoka huko iliko kwenye msimamo, vinginevyo hata kocha mwingine atakayekuja ni kumtafutia lawama tu.

Pia sikumbuki baada ya kuondoka kwa Mwenyekiti Musa Mapunda nani alibadili nafasi yake zaidi ya kuwepo Emmanuel Kimbe ambaye ni mtendaji mkuu wa timu hiyo - na pia sijawahi kufahamu tena kama ana wasaidizi ama lah.

Ni ngumu kwa timu yoyote kuwa na kiongozi mmoja tu anayebeba majukumu yote ingawa inaelezwa kwamba kuna Bodi ya Wakurugenzi, bodi ambayo haijulikani hata wajumbe ni akina nani ambao wanaweza kuipigania timu yao.

Ni vyema pia kimbe akajua kwamba nyakati ni ukuta ukishinda nao utaumia, hivyo naye apambane. Kimbe uliipandisha timu na itakufia, kwani peke yako huwezi maji yamezidi unga sasa.

 

Advertisement