UCHAMBUZI: Mwanataaluma anapoitaja shida ya maadili

Kuna kesi moja ya usajili tunatakiwa kujilazimisha kuelewa kwamba hatutaweza kuja kusikia usahihi wa hukumu yake kama ambavyo wengi wanasubiri na shida siyo vielelezo tatizo kubwa, ni wale ambao wanaitolea uamuzi kesi husika.

Niliwahi kuandika hapa kwamba kuna wasiwasi wa wazi juu ya waliopewa dhamana katika kuongoza hizi kamati wakawa si watu sahihi na wanaonyesha shaka kubwa juu ya zile zinazoitwa hukumu zinazokuja mbele ya umma.

Wasiwasi wangu naanza kuuona ulikuwa sahihi baada ya kuona na kusikia kauli moja kutoka kwa mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania akitangaza hukumu mbalimbali wiki hii katika mashauri kadhaa yaliyofika kwenye meza yake.

Hatua ya kwanza nilishtuka kumuona mwanataaluma muhimu akifika katika kamati hiyo akiwa amevaa mavazi ambayo yalishtua sana kumuona mtu mwenye nafasi kama yake akija akiwa amevalia vile - tena katika kamati nzito ya maadili akivalia kofia na t-shirt.

Achana na hayo mavazi lililonishtua zaidi ni kile alichokuwa ameshika katika mkono wake wa kushoto sigara moja kubwa hivi hapo ndipo nilipochoka kabisa na kuanza kufikiria nipo katika kuisikiliza kamati ya maadili au bonanza la mbio za mtaani?

Sikuelewa kwanini aliamua kuja vile katika mkutano ule huku akitangaza uamuzi mzito mbalimbali wa wadau wa soka, ilhali akiwa vile. Nikajiuliza hivi alishindwa kusubiri amalize kutangaza hukumu zile kisha aendelee kutumia au kushika kile anachopenda?

Nikajikuta nawauliza watu mbalimbali ambao nao walipoona wakasikitika na kuona kuna shida kubwa ya kimaadili kwa mkubwa tule tu kabla ya wale ambao aliwasomea hukumu zao pale na binafsi naona kuna haja ya kuungana nao.

Baada ya kusikia hivyo nikapata jibu la wazi kwamba kuna mambo mengi hayapo sawa na inawezekana wako wengi wanahukumiwa na kupewa adhabu ambazo hazina usahihi, lakini pia kubwa ni kwamba inawezekana kuna mambo mengi ya hivyo yanaweza kuwa yanafanyika katika kamati hizi yanaondoa haki.

Unapokuwa katika kusimamia vyombo vya haki kama hivi kuna sababu kubwa hata wanaoongoza kuwa katika usafi mkubwa sio tu wanapokuja katika macho ya watu, lakini pia hata katika yale ambayo wanayazingatia katika kutoa hukumu husika.

Kigogo huyo ameamua kututhibitishia hili kwa jinsi alivyokuja mbele yetu na kuturahishia kwamba hata katika teuzi hizi za hawa wanaoongoza kamati, bado nao wanashida kabla ya yale ambayo wanakwenda kuyatolea unyoofu.

Ipo sababu ya kuanza kwanza kuwafikiria hata wanaowachagua kuwa na upana wake katika kuwafanyia tathmini wale ambao wanapewa majukumu haya kwa kuwa sasa ni wazi tafsiri inayokuja ni kwamba uteuzi huu hautakuwa na maana ya weledi zaidi ya kuwa watu ambao wanakuja kufanya mambo yanayoacha maswali.

Kama wanataaluma wenzake wanashangaa, basi wale wadau wa kawaida nao watakuwa katika mazingira magumu zaidi kuweza kukubaliana na haya ambayo wanawapelekea kama hukumu, lakini kibaya zaidi ni wale ambao wanahukumiwa.

Hii ni shida kubwa zaidi katika mpira wetu kama hata wanaotoa uamuzi huu wanaonyesha wazi kuwa na kasoro katika mambo madogo kabla yale ambayo tunatakiwa kuyapokea kutoka kwao, ambayo tunaamini yanakuja kutokana na uamuzi wa kisheria wakiegemea katika weledi wakiwa ndani ya hivyo vikao.

Mazingira kama haya sasa nalazimika kuelewa wazi kwamba kuna shida kubwa katika hizi kamati na ndio msingi hata hukumu zake nyingi zimekuwa zikileta wasiwasi na maswali mengi - kwa wadau ambao wanasubiri kuona yale yanayotoka kwao yako sawa na hakuna mizengwe.

Ndio maana basi, ipo haja kubwa ya kuwa na watu wasafi katika kila eneo la maisha yao, hasa katika nyadhifa nyeti na zinazobeba uadilifu kama hizi.