UCHAMBUZI: Msiseme sijaawambia

Tuesday October 13 2020
CHAMBUZI PIC

HII ni siriazi. Msiichukulie kawaida Arsenal. Msimchukulia kawaida Mikel Arteta.

Msiseme sijawaambia. Kuna kitu tofauti sana kitafanya na miamba hiyo ya Emirates msimu huu. Arsenal wameshindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini huwezi kuweka sarafu yako kwenye kushindwa kukamatia tiketi hiyo kwa msimu ujao. Watoboa kwenye Top Four.

Arteta ameonyesha kuwa na ushawishi mkubwa kwenye kikosi hicho. Ameshawishi straika wake namba moja, Pierre Emerick Aubameyang kubaki. Amebaki licha ya kwamba timu zilizokuwa zikimfukuzia, Barcelona walikuwamo pia.

Ameendelea kuwa na msimamo wake kwamba Mesut Ozil si mtu anayefaa kwenye mipango yake. Hakuna anayemwingilia kwenye hilo. Arteta amekuwa na ushawishi pia kwa mabosi wake, wachezaji wote aliotaka timu iwasajili, imefanya hivyo.

Ilikuwa rahisi kuwashawishi kwa sababu kama timu imebeba Kombe la FA ikiwa na udhaifu mkubwa, vipi akipewa wachezaji anaowataka? Mabosi wameweka imani juu yake.

Usajili wa Thomas Partey umeonyesha tofauti yake na Ole Gunnar Solskjaer. Mabosi wa Arsenal wanamwamini Arteta. Amewaambia anamtaka Partey, wamemletea licha ya kwamba usajili huo umefanyika kwa kuchelewa. Solskjaer amemtaka Jadon Sancho, hajaletewa na mabosi wake.

Advertisement

Pengine wanatia mashaka juu ya uwezo wake wa kuwatumia wachezaji anaowataka. Ameletewa Harry Maguire na kiwango chake kinashuka kila kukicha. Ameletewa Bruno Fernandes na sasa kiungo huyo ameshaanza kupoteza furaha.

Ameletwa Donny van de Beek, hata miezi miwili haijapita, tayari ameanza kupaona Old Trafford sio. Solskjaer hajui namna ya kumtumia mchezaji huyo. Pauni 39 milioni hata hazijapoa, anamchezesha mchezaji dakika tatu.

Solskjaer ameingia nusu fainali tatu msimu uliopita, hakuna hata moja aliyoshinda.

Hata kwenye Ligi Kuu England, tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, amepata kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa msimu, tena kwa kuzisubiri Chelsea na Leicester City kuteleza kwenye mechi zao.

Arteta atawaonyesha kitu tofauti. Kwanza kumnasa Partey ni ushindi mkubwa kwake. Ujio wake, utamfanya acheze fomesheni ya 4-3-3 kwa kujiachia. Kushambulia ndicho kitu anachopenda Arteta.

Sasa, Partey, Granit Xhaka na Dani Ceballos watakamatia sehemu ya kiungo, wawili watakuwa na kazi ya kuwalinda mabeki wa kati na mmoja atakuwa bize kuwachezesha washambuliaji.

Arteta anaamini kwa kumpata Partey basi atakuwa amemaliza ile shida iliyosumbua timu yake. Ameleta jiwe hilo kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja. Arteta hajafanya usajili wa kupaniki. Willian anafanya vizuri kabisa kwenye kiungo ya pembeni na Gabriel ameleta utulivu mkubwa kwenye beki.

Kwa uhodari wa Arteta na usajili huu aliyofanya kuboresha kikosi chake, kuna jambo kubwa linaweza kufanywa na Arsenal kwa msimu huu na kuwarudishia mashabiki furaha iliyokosekana miaka mingi.

Arteta hakusajili kundi kama alivyofanya Frank Lampard huko Chelsea. Ametibu maradhi yanayosumbua kikosi chake. Na sasa, unakwenda kuwakabili Arsenal usiende kichwakichwa, nenda kwa nidhamu kubwa.

Nimeziona Liverpool, Man United, Man City, Spurs na Chelsea kwenye mechi zao walizocheza kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, unaona dhamiri kabisa kuna upenyo mkubwa wa Arsenal kupenya na kutamba katikati yao msimu huu.

 

Advertisement