UCHAMBUZI: Miujiza haitaisha kwa Zlatan Ibrahimovic

BILA ya shaka umeshawahi kusikia Ibrahim Ajibu akiitwa Ibra Cadabra.

Hii inatokana na jina lake la Ibrahim kufanana na lile la Ibrahimovic (Zlatan) ambaye kimsingi ndiyo mwenye jina la Ibra Cadabra.

Kwa kuwa Ajibu ni Ibra na Zlatan ni Ibra... wabongo wakahamisha jina. Sisi wabongo!

Lakini kimsingi Ajibu hakupaswa kuwa Ibra Cadabra, kwa sababu hana hizo sifa. Zlatan ndo mwenye sifa stahiki.

Kwanini? Asili hasa ya jina Ibra Cadabra ni neno ABRA CADABRA ambalo maana yake ni sanaa ya mfanya mazingaombwe kuongea maneno mengi ambayo hayaeleweki.

Kama ulibahatika kuona mazingaombwe utakuwa ulimsikia ‘ndugu mtaalamu’ akibwabwaja maneno mengi ambayo hayajulikani ni ya lugha gani.

Sasa ile bwabwaja bwabwaja yake ndiyo huitwa ABRA CADABRA.

Ndio maana nasema, Ajibu hastahili kwa sababu hana maneno mengi...hajui kubwabwaja, lakini Zlatan, mtakesha.

LIMEISHIA WAPI?

Kuna nadharia inayosema kwamba neno hili lilianza baada tu ya kusambaratika kwa mnara wa Babel ambapo kila mtu alijikuta akiongea lugha anayoijua yeye.

Kwa hiyo kila mmoja akawa anafanya abra cadabra...na vitabu vinasema hapo ndipo lugha mbalimbali zilipozaliwa.

Neno hili lina asili ya lugha ya Aramaic yaani Avrah KaDabra, likiwa na maana ya NITAUMBA KAMA NINAVYOONGEA - likirejea muujiza wa Mungu wakati wa uumbaji, ambapo aliumba kwa kusema KUWA na IKAWA!

Aramaic ni lugha ya kale ya Mashariki ya Kati ambayo ni jamii ya lugha kama Kiebrania, Kiarabu na lugha nyingine nyingi za eneo lile.

Wafanya mazingaombwe walihusishwa na neno hili kwa sababu hufanya miujiza yao kama ya uumbaji, kwa kusema sema tu.

Zlatan Ibrahimovic alipewa jina hili kwa sababu mbili.

Mosi, akiwa uwanjani hufanya miujiza mingi katika uumbaji wa mabao.

Pili, akiwa nje ya uwanja huongea maneno mengi kama mfanya mazingaombwe.

Kwa kuwa neno lenyewe linaanzia na ABRA na yeye jina lake linaanzia IBRA, basi ile Abra ikachakachuliwa na kuwa Ibra...ikawa Ibra Cadabra badala ya Abra Cadabra.

Katika lugha ya ulimwengu wake, uchakachuaji wa aina hii yeye huuita kuzlatani...kwa hiyo ile Abra ikazilataniwa na kuwa Ibra...na kuzaliwa Ibra Cadabra.

Na ndio maana hata nchi yake ya Sweden, yeye ameizilatani na kuiita Zweden...katoa S, kaweka Z ya kwenye jina lake la Zlatan!

I. MIUJIZA YA UUMBAJI MABAO

Akiwa na umri wa miaka 39, Zlatan Ibrahimovic bado ana uwezo wa kupambana katika kiwango cha juu kama kijana wa miaka 20.

Fikiria kwenye mchezo wa upinzani wa jadi wa jiji la Milan, Inter Milan dhidi ya Milan, Zlatan anawafunika vijana kama kina Romeru Lukaku na kufunga mabao mawili yanayoamua mchezo kwa ushindi wa timu yake wa mabao 2-1.

Anasema: “Kwenu nyote mnaodhani nimekwisha ndiyo kwanza napasha misuli moto.”

Yaani Zlatan bado anajiona kama anaanza, akiwa na miaka 39 ilhali vijana wa miaka 20 na kidogo wameshaanza kuzeeka.

Novemba 2019, Dele Alli wa Tottenham Hotspur alisema ameanza kuzeeka hivyo mwili wake kuna vitu unashindwa kuvifanya. Wakati huo alikuwa na miaka 23.

II. MIUJIZA YA MANENO MENGI

Mwishoni mwa mwezi Septemba zilitoka taarifa kwamba Zlatan amepatikana na maambukizi ya maradhi ya Covid 19, lakini yeye mwenyewe akaingia Twitter na kusema: “Jana nilikuwa sina virusi, leo eti ninavyo. Hivi virusi vimepata wapi ujasiri wa kunijaribu? Wazo baya kabisa.’

Yaani Zlatan alishangaa kwamba virusi vilipata wapi kiburi cha kumjaribu yeye?

Yaani katika mawazo mabaya ambayo virusi hivyo vimeshawahi kuwaza, basi ni kwenda kwa Zlatan.

Watu wengi wakajitokeza na kuvipa pole virusi kwamba sasa vitakiona cha moto.

Gary Lineker, mfungaji bora wa Kombe la Dunia 1986 ambaye sasa ni mtangazaji wa BBC, akasema, ‘maombi yetu na mawazo yetu yote ni kwa virusi’.

Hii ni kauli ambayo hutolewa kwa mtu aliyepatwa na matatizo makubwa...kwa hapa Lineker aliviona virusi kuwa vimepatwa na matatizo makubwa sana.

Mwanzoni mwa Oktoba ikatoka taarifa kwamba Zlatan hana tena maambukizi.

Badala ya kusema Zlatan amepona ugonjwa virusi vya corona, ikawa virusi virusi ndiyo vimepona ugonjwa wa Zlatan.

Miujiza haitoisha kwa Zlatan.