UCHAMBUZI: Mashabiki kupigana elimu itolewe kwa wasemaji

Moja kubwa lililobamba vichwa vya habari wiki iliyopita ni mwendelezo wa mashabiki hasa wale wa klabu za Simba na Yanga kuonyeshana umahiri wa kutibuana majukwaani na hata kupigana.

Matukio hayo yamekuwa yakichafua taswira nzuri ya kiwango cha nidhamu na mashabiki kuheshimiana, na hata kuishi kama kitu kimoja licha ya tofauti ya hisia kwa klabu zao - kwa maana ya kile mtu anapoamua kuchagua klabu ipi aipende.

Sio matukio mapya, lakini taratibu wapo ambao wanadhani kumpiga shabiki wa Yanga au Simba, basi unaonekana ndio unaipenda sana klabu yako na kuacha kupambana na mambo ya msingi yenye afya kwa kila mmoja na klabu yake.

Klabu zote mbili hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekemea tabia za namna hii na kuwataka mashabiki wao kuwa mfano mzuri wa kuishi kwa upendo na kuheshimiana kuliko kushambuliana.

Hii sio mara ya kwanza kwa klabu hizi kukemea matukio ya namna hiyo, lakini licha ya matamka yote hayo mambo yameendelea kuwa yaleyale ya kushindwa kuheshimiana wanapokutana majukwaani.

Kuna eneo linasahaulika kulifanyia kazi na watu wanashindwa kufanya tathmini fupi kwa kazi za maofisa habari wa klabu hizi mbili.

Kwanza niwapongeze maofisa habari kwa kufanya kazi zao na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi wanazozifanyia kazi, lakini yapo ambayo pia wanayakosea na kuzidi kuchagia kadhia ya namna hii.

Shida kubwa ambayo naiona kwa wasemaji baadhi wamekuwa sio wasemaji wa klabu zao, na muda mrefu wamekuwa na hulka ya kupenda kuzisema vibaya klabu pinzani na kushindwa kuelewa kwamba hatua hiyo baadaye inazaa kitu kibaya.

Kuwa msemaji wa Yanga hakutakuwa na maendeleo kwa klabu yako eti kwa kuamua kuisema vibaya Simba zaidi - kwa kuichafua zaidi lakini pia kinyume chake hauwezi eti kuonekana unaisema vibaya Yanga kwa maneno makali kisha ukaonekana unafanya kazi yako vyema.

Hatua hii imekuwa ikionekana kwamba msemaji anayekuwa bora eneo hilo ndiye anaonekana bora na mashuhuri kushinda mwingine, lakini linapokuja suala cha changamoto hapo ndipo inakuja shida.

Msemaji anapoisema vibaya timu pinzani kwa hatua ya kuudhi hapo ndipo tunapopandikiza chuki baina ya mashabiki na hatua inayofuata ni kushuhudia vituko vya kudhalilishana kama ambavyo miaka ya sasa vimekuwa vikishamiri.

Shida kubwa ni kwamba hata TFF wako kimya na wameshindwa kuwakumbusha wasemaji hao juu ya majukumu yao ya msingi katika maelekezo ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa), ambao ndio waliotoa maelekezo ya watendaji hawa kutakiwa kuwepo ndani ya sekretarieti za klabu.

Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiitana majina makali ya kuudhi, na pia zipo hata lugha ambazo zinaashiria matusi zimekuwa zikitolewa, lakini inaonekana wakubwa nao wameafiki hayo na maisha yamekuwa yakiendelea.

Kumbuka wakati klabu hizi zilikuwa na wasemaji kama Luis Sendeu pale Yanga na kule Simba kulikuwa na Ezekiel Kamwaga wakati pale TFF kukiwa na mtu makini Boniface Wambura maisha ya kuchafuana na kudhalilishana hayakushamiri kama sasa.

Hatua nzuri ni kwamba, TFF ni mashahidi wazuri katika kuona upungufu mkubwa wa wasemaji hawa kutoka nje ya majukumu yao ambapo tumeshuhudia wamekuwa wakipigwa faini mbalimbali kutokana na matamshi yao.

Tumekuwa tukizilea klabu hizo mbili, hivyo kwa kushindwa kusimamia vyema nidhamu ya wasemaji hawa sasa tunakwenda kuharibu utulivu wa mpira mzima kwa mashabiki kupandikiziwa chuki.

Ni wakati wa kujitafakari. Naona kabisa chanzo kikubwa cha mmomonyoko huu ni hatua ya kupandikiziwa chuki baina ya klabu kwa klabu - kazi ambayo inafanywa na wasemaji na si vinginevyo na sidhani kama wapo viongozi wengi wa klabu hizi wanavutiwa na hili kwa mashabiki kuendelea kutenganishwa na kuondolewa umoja wao.

Utani wa hizi klabu ni tofauti kabisa na maisha ya sasa. Utan wao unapaswa kuwa katika kusaidiana kwenye shida na raha, lakini pia kutaniana ila sio kuchafuana kama ambavyo inatokea sasa.