UCHAMBUZI: Hili la mashabiki kupigana liangaliwe kwa mapana

Hivi sasa inadaiwa mashabiki wa Yanga ndio wanaodaiwa kuongoza kwa kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba mara tu wanapokuwa uwanjani, hasa wanapokwenda kutazama mechi ambazo Yanga wanacheza.

Kwa kawaida imezoweleka kuwa Simba na Yanga mashabiki wao hujitenga wawapo uwanjani, ingawa kuna wachache hukaa kwenye majukwaa ya wapinzani wao, iwe Simba au Yanga.

Hali inapokuwa hivyo ni lazima kutokee kelele za kuwaamuru waliokaa upande wa wenzao waondoke ambapo hurushiana maneno ya utani kama ilivyo kawaida na huo ndio utani wao.

Wanasema utani sio uadui, mnataniana kimpira halafu maisha mengine yanaendelea ingawa hivi sasa jambo hilo sio rahisi kulikuta kwa baadhi ya mashabiki ambao wamegeuza utani kuwa uadui.

Tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara uanze ni mara mbili imetokea mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu wenzao ambao wanaenda kukaa eneo lao pale ambapo wanaangalia mechi zao.

Wanafanyiwa fujo kwa sababu tu wanakuwa wamevaa jezi za Simba na hivyo kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ni mashabiki wa Simba na kuanza kufanyiwa vitendo hivyo ambavyo sio vya kiungwana katika soka.

Baada ya vurugu zilizotokea Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kila mamlaka inayojihusisha na soka imetoa tamko la karipio kali na kuacha jambo hilo mikononi mwa dola ili vifanye kazi yao.

Baada ya video ile kusambaa mitandaoni, uongozi wa Yanga ulitoa tamko kisha ikafuata Bodi ya Ligi iliyotoa tamko na kuitaka Yanga kuhakikisha inachukulia hatua vinginevyo hatua kali zitachukuliwa juu yao.

Simba nao walitoa tamko kwa kufuata taratibu zao, ambapo wamezungumza kwanza na wenzao Yanga na baadaye wakaandika barua Bodi ya Ligi na TFF kueleleza namna gani wanasikitishwa na vitendo hivyo na kuwaomba kuchukua hatua inayostahiki kwa wanaofanya vurugu.

Simba wametumia pia uungwàna kwa kuwataka mashabiki wao kutolipa kisasi kwa mashabiki wa Yanga, bali waendeleze umoja na mshikamano pamoja na utulivu ndani ya timu yao.

Wote wamezungumzia vurugu hizo kwa kukemea na kuliacha jambo hili mikononi vya vyombo vya dola ili vikiwabaini wanaofanya vurugu washughulikiwe kama waharifu wengine kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mengi sasa hivi yanaendelea kwenye mitandao ya kijamii kwa kutoa vitisho mbalimbali ambapo video zinazoonyesha kuwa ni mashabiki fulani wanazungumza wazi juu ya kufanya fujo.

Wanasaokolojia wamezungumza kuwa tatizo linalosababisha mashabiki hao kufanya vurugu ni kuwa na imani kubwa na timu yao kufanya vizuri, lakini matokeo wanayokutana nayo ni tofauti na matarajio hivyo wanapata hasira.

Lakini sidhani kama kuna sababu ya kufika huko wakati inajulikana wazi kwamba kikosi cha Yanga kwa asilimia kubwa kina wachezaji wengi wapya na muda wa maandalizi ulikuwa mdogo, hivyo wanatarajia kupata matokeo ya aina gani kwa kipindi hiki.

Ni lazima wakubali kujipa muda wa kuanza kupata matokeo mazuri ingawa wao huenda wanachokihitaji ni kuona timu yao inafunga mabao mengi na si kusondosha bao moja moja.

Mashabiki wa Yanga huenda wanaona wivu na namna ambavyo watani zao wanapojikusanyia mabao mengi kwenye mechi moja tofauti na wao pasipo kuangalia kikosi cha Simba kimekaa pamoja kwa kipindi gani. Simba hawapo katika wakati wa kutengeneza kombinesheni kama ilivyo kwao.

Hivyo ni suala la muda kwa mashabiki wa Yanga kuwa na subira katika matokeo yao yanayopata hivi sasa kikubwa washukuru wanapata hata hizo pointi tatu ambazo wachezaji wao wanazipigania kwa nguvu kubwa.

Ni jukumu la mashabiki wa Yanga kuachana na hayo mambo badala yake waiunge mkono timu yao kuhakikisha wanatoa hamasa kubwa ya kuwatia moyo, kwani ipo siku wakiendelea kufanya vurugu watafungiwa kuingia uwanjani na wachezaji wao watalazimika kucheza pasipo kupata sapoti ya mashabiki wao.

Tunaamini sheria zipo wazi tu ingawa sasa inaonekana viongozi wa soka wanachukulia uungwana ndio maana wanasisitiza uongozi wa Yanga kuchukua hatua maana wanajua madhara yake kama watachukua hatua kali zaidi juu yao.

Mashabiki wa Yanga huu si wakati wa kufanya vurugu kisa tu shabiki wa Simba amekaa upande wenu, utu utumike katika kushabikia timu zenu kwani ikiachwa hivi kuna siku madhara makubwa yatatokea.

Ni vyema sasa mashabiki wote wa soka pamoja na michezo mingine wakajielekeza zaidi katika kuonyesha utu, uzalendo na mapenzi kwa timu na michezo wanayoishabikia badala ya kugeukiana wao kwa wao kuharibiana siku - kwa kupigana.Michezo sio uaduli, bali burudani.