UCHAMBUZI: Bosi TFF aandaliwe hotuba ili kumsitiri

Jumanne ya Oktoba 6, mwaka huu, Shirikisho la soka nchini (TFF) lilisaini mkataba wa miaka mitatu wa udhamini wa timu ya taifa, Taifa Stars wenye thamani ya Sh3 bilioni.

Sitaki kujikita kwenye mkataba huu, bali kwenye kauli ya rais wa TFF, Wallace Karia aliyoitoa akielezea mafanikio ya Taifa Stars chini yake.

“Sikimbuki lini mara ya mwisho Tanzania iliingia hatua ya makundi kufuzu Kombe la Dunia.” Hii ndiyo kauli inayonifanya nimuone Karia anakuja, anakataa...anakuja anakataa!

Ni kweli kwamba chini ya utawala wake tumeshuhudia maendeleo makubwa sana ya kitaasisi, kiufundi na matokeo, akini kuingia hatua ya makundi siyo kitu kigeni kwetu na wala si mafanikio kwa sababu tumekuwa tukiingia hatua ya makundi mara kwa mara.

Kufuzu Kombe la Dunia 2010 tulikuwa kundi namba moja tukiwa na Cameroon, Cape Verde na Mauritius, tukaambulia nafasi ya tatu.

Mashindano haya ya kufuzu kombe la kwanza kufanyika barani Afrika, yalienda sambamba na kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Afrika Afcon- 2010 nchhini Angola.

Pia kufuzu Kombe la Dunia 2014 tuliingia hatua ya makundi na tukawa pamoja na Ivory Coast, Morocco na Gambia tukashika tena nafasi ya tatu (kama ilivyo katika chati juu-kulia).

Moja ya mechi za kukumbukwa ni dhidi ya Morocco ambayo tuliwafunga 3-1 hapa nyumbani na kutufunga kwa mbinde 2-1 kufuatia kadi nyekundu ya mapema (dakika ya 38) ya Agrey Morris.

Ni Kombe la Dunia la 2018 pekee ndilo tuliloshindwa kutinga hatua ya makundi tulipotolewa na Algeria kwa aibu.

Lakini rais wa TFF hakukumbuki mara ya mwisho lini kutinga hatua ya makundi.

Tanzania ilitinga hatua ya makundi kufuzu Kombe la Dunia 2022, Septemba 2019 kwa kuwatoa Burundi.

Kulikuwa na muda wa kutosha kufanya utafiti na kujiridhisha ili isitokee aibu kama hii.Hapa ndipo kwenye umuhimu wa kuandikiwa hotuba ili ‘maboko’ kama haya yaepukike.

Wanaomzunguka kuanzia makamu wake, katibu mkuu na hata kurugenzi ya habari wawajibike katika kumuandaa mkuu anapotaka kuongea.

SIYO MARA YA KWANZA

Ukurasa huu umeshawahi kuandika mara mbili juu ya kauli za rais wa TFF, zinazoonyesha aidha umuhimu wa kuwa na kumbukumbu nzuri au kutojua kwa undani mambo yanayolizunguka soka.

Katika toleo la Machi 16, 2018 chini ya kichwa cha TATIZO LA KARIA NI WANAOMZUNGUKA, ukurasa ulijaribu kuifananisha TFF ya Karia na serikali ya kufikirika ya waziri fulani.

Hiyo ilifuatia kauli aliyoitoa Jumatano ya Desemba 27,2017 kwenye Hoteli ya Sea Scape One alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari za michezo. Ilikuwa takribani wiki moja tangu Fifa itoe viwango vipya vya mwezi Desemba vilivyoonyesha Tanzania kushuka kwa nafasi tano chini kutoka nafasi ya 142 mpaka 147.

Mhariri mmoja akamuuliza rais Karia juu ya kuporomoka kwa Tanzania, yeye akawa na jibu rahisi kabisa kwamba Tanzania imeshuka viwango kwa sababu haikucheza mechi yoyote tangu viwango vya mwisho vya Fifa vya Novemba vitolewe.

Akasisitiza kwamba mechi pekee ambayo Tanzania ilicheza ni za mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo hayana uhusiano na kuporomoka kwa viwango vya Tanzania kwa sababu Fifa hawayatambui.

Rais Karia alikuwa hajui kama Fifa inayapa mashindano ya Cecafa hadhi sawa na mechi za kirafiki za kimataifa zilizopo kwenye kalenda ya Fifa.

Matokeo mabovu ya Tanzania kwenye Cecafa ndiyo yaliyowekwa kwenye tovuti ya Fifa kama mrejeo wa Tanzania kuporomoka kwa mwezi Desemba.

Akairudia tena kauli hii Februari 13, 2018 wakati wa mkutano wa Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa watu maalumu Uwanja wa Uhuru kuelekea ujio wa rais wa Fifa, Giani Infantino.

Hata kwenye mazungumzo ya kawaida baada ya Stars kuvurunda kwenye ile Cecafa ya Kenya huku kocha akitutaka Watanzania kukaza ulimi ili kuongea Kiingereza, bosi wa TFF alikuwa akisisitiza kwamba Watanzania wasiumizwe sana na matokeo yale kwa sababu hayana maana yoyote zaidi ya kujifurahisha tu.

Kama tungeshinda mchezo wetu na Burundi Jumapili, basi tungepata pointi za viwango vya Fifa, sawa na zile ambazo tungezipata kwa kushinda mchezo wowote wa mashindano ya Cecafa.