Tyson vs Evander III mzuka ndio unarudi upya

VUTA picha umetulia zako na kinywaji chako mkononi, ghafla unasikia kwamba wababe wa dunia wa enzi hizo, Mike Tyson na Evender Holyfield wanarejea ulingoni. Kisha fikiria hapo ulingoni patakuwaje. Zile kambi za kibabe za hawa wateni na waliotesa kwa muda mrefu kwenye masumbwi watakuwa wamesimama watu gani?

Ndio, ni rasmi kuwa Tyson mwenye miaka 53 kwa sasa na Evander, ambaye ana miaka 57, kila mmoja ameweka bayana kwamba, anataka kurudi ulingoni kwa shoo moja tu ya kumaliza ubishi nani zaidi.

Haya unaweza kuyaita maajabu kwani, ni miaka 23 sasa tangu wababe hawa walipopanda kuzichapa na pambano kusiha kwa vurugu. Sasa Tyson na Evander wameamua kuonjesha kizazi cha sasa, nini maana halisi ya ngumi za uzito wa juu.

Kabla mwaka kumalizika, dunia hii iliyoamua kujifungua kwa hofu ya corona, inakwenda kuonja ladha ya kile kilichotokea Novemba 9, mwaka 1996 kwenye ukumbi wa MGM Grand Garden Arena pale Las Vegas, Marekani. Dunia bado haijasahau usiku wa ‘The Bite of 97’. Katika miongo mitatu ulimwengu wa masumbwi ulishuhudia wababe hawa wakirekodi jumla ya mapigano 115. Katika miongo hiyo kizazi hiki kinachowashangaa kina Anthony Joshua, hakikuonja balaa la Tyson na Evander.

Kwa wiki mbili sasa, wakongwe hawa wamekuwa wakifanya mazoezi ya nguvu, kuajiandaa na pambano hili, ambalo wengi wanaamini litasimamisha dunia kwa sekunde kadhaa. Wengi wanasubiri kuona makonde halisi na sio maigizo kama ya kina Floyd Mayweather Jnr.

MZUKA WA PAMBANO

Mtu wa kwanza kuthibitisha hitaji la kurejea ulingoni ni ‘King of Cannabis Empire’ Mike ‘Iron’ Tyson. Aprili 24, bingwa huyo wa zamani wa uzani wa juu, alisema: “Nimekuwa nikifanya mazoezi kwa muda wa wiki mbili sasa.

“Mwili wangu unaonyesha kuhitaji kitu. Nataka kupata mapambano kadhaa ya hisani, najua kwa njia hiyo, angalia nitatoa mchango wangu kwa jamii. Naamini bado naweza kupigana, niko tayari.”

Siku chache baadaye, mpinzani wake mkubwa, Evander, licha ya kuwa na umri mkubwa wa miaka 57, pamoja na mwili wake kuonekana pia kukosa nguvu, alikiri yuko tayari kurejea ulingoni. Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kupigano na Tyson, alisema:

“Kwanini nikatae. Niko tayari kupigana na Tyson muda wowote. Nina miaka 57, lakini najua niko fiti, lakini kitu cha kujiuliza ni je, Tyson yuko tayari kupigana na mimi?” alisema Holyfield na kuendelea.

“Jambo la kuzingatia ni kwamba, hatupigani kupata mshindi. Hatushindani, lakini tunapigana kuonyesha kizazi hiki, kuwa huko nyuma tulikuwepo na tulipigana hasa. Hii sio mechi ya kulipiza kisasi, tunarudi ulingoni kufanya kitu kizuri kwa ajili ya jamii.”

PAMBANO LENYEWE

Bado haiwekwa wazi kama pambano hili litafanyika kweli ama la. Lakini, tetesi zinasema huenda wazee hawa watakumbukiwa ujana wao, katika moja ya kumbi za kifahari zilizoko ndani ya jangwa la kifalme, huko Diriyah, Saudi Arabia.

Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zinaashiria kwamba, huenda dunia ikashuhudia uhondo huu mapema Julai 11, usiku na dunia inasubiri kwa hamu kunbwa.

PAMBANO LA MWISHO

Kuna kitu ambacho dunia inakitafuta. Ndio maana inawalazimisha wababe hawa kurudi ulingoni. Sio kupenda wao, lakini ni hitaji la kukata kiu. Walipokutana mara mbili, Tyson alilamba sakafu. Ilikuwa ngumu kuamini hilo.

Mara ya kwanza kukutana, ilikuwa ni mwaka 1996. Kila mtu aliamini Holyfield angetupa taulo, lakini haikuwa hivyo. Katika raundi ya 11, Tyson baada ya kula ngumi za kutosha, aliomba poo. Mwanaume alipigwa kwa TKO.

Dunia ilikataa kukubali. Mwaka mmoja uliofuata, Juni 28, mwaka 1997 ndani ya MGM Grand Garden Arena huko Nevada, pakapigwa tena shoo nyingine ya kibabe sana maarufu kama ‘The Sound and the Fury’

Katika pambano hili, ambalo baadaye lilikuja kuwa maarufu kwa jina la ‘The Bite Fight’ au ‘The Bite of ‘97’, Tyson aliadhibiwa kwa kosa la kumng’ata Holyfield sikio hadi likakatika kipande. Matokeo yake, majaji na waamuzi wakamtunuku Holyfield ushindi wa mezani ambao, kwa baadhi hawakufurahi nao.

ILIKUAJE KABLA YA KUSTAAFU?

Holyfield aliyezaliwa Oktoba 19, 1962, aliingia ulingoni kuanzia mwaka 1984 hadi 2011, alipostaafu. Holyfield ‘The Real Deal’, ambaye ni bondia pekee aliyetesa kama Undisputed Champion katika mapambano mawili tofauti, hakustaafu kwa heshima kama ilivyotarajiwa.

Licha ya kuwa na rekodi ya kutwaa ufalme wa uzito wa juu (World Heavyweight), mara nne, alishindwa kutetea mkanda wake dhidi ya Lennox Lewis. Walikutana mara mbili, katika pambano la uzito wa juu (unified WBA, WBC na IBF), pambano la kwanza, likamalizika kwa sare (1999).

Pambano la marudiano lililofanyika miezi nane baadaye, akasalimu amri. Mwaka uliofuata alimtandika John Ruiz na kukamilisha idadi ya mataji manne ya World Heavyweight. Hii ilikuwa rekodi ambayo haijafikiwa mpaka sasa. Miezi minne baadaye, alitandikwa vibaya na Ruiz.

Holyfield, aliyetangaza kustaafu Juni 2014, baada ya kukaa nje ya ulingo kwa miaka mitatu, alitwaa unified WBA, WBC na IBF (1990-92), ubingwa wa WBA na IBF (1993-94), ubingwa wa WBA mara tatu (1996-99) na IBF mara tatu (1997-99), na ubingwa wa WBA mara nne (2000-01).

Kwa upande wake, Tyson, alistaafu mwaka 2006. Kama ilivyo kwa Evander, naye hakustaafu kwa heshima. Tena tofauti na Evander, Tyson alidhalilishwa na bwana mdogo mmoja hivi, asiyekuwa na rekodi nzuri kwenye masumbwi.

Baada ya kuchapwa, Tyson aliamua bora yaishe. Pambano lake la mwisho alipigana akiwa na miaka 38. Ilikuwa ni miezi 11 baada ya kukumbana na kipigo kutoka kwa Muingereza Danny Williams. Jumla ya watazamaji 20,000 walikusanyika kwenye ukumbi wa MCI Arena.

Miongoni mwa waliohudhuria, ni mfalme wa masumbwi duniani, Mohammad Ali (marehemu) na mwanaye Leila Ali. Dunia ilimtegemea Tyson kumtandika Kevine McBride ‘The Journeyman’, raia wa Ireland kwa KO. Haikuwa hivyo na hawakuamini kilichotokea!

Rekodi ya McBride. Aliyekuwa na miaka 32 (wakati huo). Haikuwa ya kuridhisha kivile. Katika mapambano yake yote 32 aliyoshinda, alitoka kupambana na vibonde, hakuwahi kukutana na shughuli ya Tyson na wakali wenzake. Hilo lilikuwa pambano lake la kwanza. Mpambano ulipoanza, McBride alionyesha kujituma sana, akirusha ngumi za haraka huku Tyson yeye akionekana kuishiwa nguvu hata kabla raundi ya kwanza haijamalizika. Mwisho wa siku, tofauti na matarajio ya wengi, Mende iliangusha kabati.

Katika raundi ya sita, ambayo ilikuja kuwa safari ya mwisho ya Tyson, kwenye masumbwi. Akiwa amejawa na hasira kutokana na kuzidiwa ujanja na McBride, ‘Iron Mike’ aliukamata mkono wa mpinzani wake, akauzangusha kwa nia ya kutaka kuuvunja.

McBride alipiga kelele, akilalamika kuhisi maumivu. Tyson alipewa karipio lakini kwa bahati nzuri, kama ilivyokuwa kwa Francois Botha, hakuadhibiwa. Muda mfupi baadaye, alianza kumtandika mpinzani vichwa, safari hii akipokonywa pointi mbili na mwamuzi Joe Cortez.

Hapa ndipo, alipokosea. Pointi hizo mbili, zilimpatia McBride kiburi cha kuanza kumshambulia kwa Uppercut mfululizo.

MAISHA BAADA YA KUSTAAFU

Baada ya kuchapwa. Baada ya kupata anguko la aibu mbele ya watazamaji 20,000. Tyson alitangaza kustaafu. Ilikuwa ni mwaka 2006. Kwa kauli yake alisema: “Naamini nitapata kazi nyingine ya kufanya, ubondia haunifai tena kwa sasa.”

Ni kweli, kwa zaidi ya miaka 15, tangu arushe taulo, Tyson amekuwa mfanyabiashara mkubwa, mcheza filamu na mkulima wa zao la bangi.

Licha ya kumpoteza binti yake wa miaka minne, Tyson alifanikiwa kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Lakiha ‘Kiki’ Spicer.

Kwa upande mwingine wa shilingi, maisha hayajamheshimu sana bingwa wa zamani wa dunia, Holyfield. Hadi kufikia Juni 2008, kulikuwa na taarifa kuwa anadaiwa deni la zaidi ya dola milioni 10, lakini ripoti ya mwaka jana, inaonyesha anaingiza dola 1.2 milioni kwa mwaka.

Hata hivyo, Holyfield umri umemtupa mkono na kuna taarifa kuwa anasumbuliwa na matatizo yanayofananiwa yale yaliyomkumba mfalme wa ngumi, Mohammed Ali (Ugonjwa wa Packinson), japo haijathibitishwa.