Tyson Fury atamba kutopigwa hadi kustaafu

HABARI ndio hiyo! Mwenyewe ameshasema huyo kwamba hana mpango wa kuachia mikanda aliyonayo ya ubingwa wa uzani wa juu duniani na kila atakaouchukua ataibeba hadi atakapotangaza kustaafu mchezo wa ngumi akituma ujumbe kwa wapinzani wake wanaowaza kupigana naye.

Sio mwingine ni Muingereza Tyson Fury,bondia huyu anayesakwa na mabondia tofauti ambao wanachukulia mfano wa “mti wenye matunda kupigwa mawe” ili kupata wanachokitarajia ndivyo ilivyo ambapo mabondia Anthony Joshua,Dylian Whyte na Deontay Wilder kwa pamoja wanapiga dua zao za kutosha tu ili wapigane naye.

Tyson aliyemvua mkanda bondia aliyekuwa kwenye ubora wake,Wladmir Klitschko kwa pointi mnamo mwaka 2015 na baada ya droo kwenye pambano la kwanza mwaka 2018 dhidi ya Deontay Wilder,alimvua Mmarekani huyo mkanda wa WBC uzani wa juu zaidi uliokuwa unashikiliwa na bondia huyo kwa miaka mitano,mwezi februari mwaka huu katika pambano la pili.

Ili kuonyesha kwamba amezaliwa kuwa bingwa kwenye ngumi akisisitiza kuwa hapigani kwa ajili ya pesa,umaarufu wala kushinda tu mikanda bali anapigana kwa ajili ya furaha na kuwa fiti zaidi akiweka wazi kuwa anataka kuwa bingwa kwa muda mrefu akimtolea mfano Klitschko aliyedumu kwa muda mrefu na kwake atastaafu bila kupoteza pambano.

Kuna uwezekano mkubwa sana Tyson Fury akarudiana na Deontay Wilder katika pigano la tatu kwa mujibu wa mkataba walioandikishana na tayari Tyson ameshathibitisha kwamba ataanza na Wilder ammalize ndipo atapigana na Anthony Joshua.