Tyson Fury afunguka kurudiana na Deontay Wilder

Muktasari:

Fury hajapoteza pambano lolote tangu aanze kucheza ngumi za kulipwa, akiwa ameshinda mara 30,  na kutoa sare 1.

LONDON, ENGLAND. BINGWA wa uzito wa juu Duniani Tyson Fury amesema kuwa   mpambano wake wa tatu dhidi ya Deontay Wilder utakuwa ni mgumu na wenye ushindani mkubwa, kutokana na kiu ya kisasa aliyokuwa nayo mpinzani wake  baada ya kumchakaza katika pambano lililopita.

Fury alimpiga Wilder katika pambano la uzito wa juu wa Dunia (WBC), Februari mwaka huu, ambapo hadi kufikia raundi ya saba tayari Wilder alishaanguka chini mara mbili, baada ya  pambano lao la kwanza kumalizika kwa sare.

 Kwasasa  Wilder anajiandaa kwa ajili ya pambano wa tatu wa marudiano akiamini kuwa litakuwa na ugumu wa aina yake.

"Bado ni mpinzani mkubwa na hatari, ambaye atakuja ili kuthibitisha kuwa yeye ni bora na anaweza kurudi kwenye nafasi yake na akawa bingwa wa Dunia kwa mara ya pili, pambano letu la tatu litakuwa ni la hatari zaidi ya yote yaliyopita'' alisema Fury

"Lakini unajua nini? Mimi naingalia kama ni mechi ya ngumi ya kawaida tu, siwezi kusema naifikiria sana, unaweza ukabahatika kushinda ama kupoteza" aliongeza.

Pambano hilo la tatu la marudiano kati ya mabondia hao wawili, linatazamiwa kwenda kupiganwa  nje ya Marekani na Uingereza kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Naangalia mbele zaidi kuhakikisha nashinda kwenye pambano hilo, haijalishi wapi utakapochezewa, nafanya mazoezi kuhakikisha nakuwa bora kwa wiki kadhaa kabla sijaenda kucheza  nae ulingoni mbele ya Dunia kwenye pambano letu baada ya janga la corona kumalizika" amesema Fury

" Jambo zuri ni kwamba, hakuna aliyedhurika wote  tumetoka uwanjani salama, na kurudi kuungana na familia zetu, hali inayoashiria kuwa tutakuwa na pambano lingine na lenye ushindani''

Tofauti namimi  sidhani kama kutakuwa na mtu mwengine  atakayeweza kukatiza mbele yangu na kutamba kwenye mchezo wa  ngumi, naamini kuwa mimi ndio mfalme wa mchezo huu, na hakuna mwingine atakayekuja kuvaa taji hili. Hakuna kabisa,” alisema

Fury  ambaye anashika nafasi ya kwanza ya ubora kwa mabondia wa uzito wa juu, ameshinda jumla ya mapambano 30, huku 21 yakiwa ni kwa KO na kutoka sare pambano moja, wakati akiwa hajapoteza pambano hata moja, katika jumla ha mapambano 31aliyocheza.