Twiga Stars ijipange tu

Muktasari:

Wakati Twiga Stars ikijifua kuna mataifa ambayo yana rekodi matata na tishio kwa timu za wanawake Afrika.

TIMU ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ inatakiwa kujifunza kupitia mataifa ambayo yana rekodi ya kufanya vyema katika michuano ya kimataifa wakati wa maandalizi yao ya kujiandaa na michezo mbalimbali wanayotarajia kushiriki.

Hivi karibuni kocha wa timu hiyo, Bakari Shime alitangaza kikosi cha wachezaji 40 ambacho kitaingia kambini Septemba 21 mwaka huu ili kujiwinda na michuano mbalimbali.

Kikosi hicho na timu wanazotoka wachezaji katika mabano kinaundwa na Najat Abas (JKT), Tausi Abdallah (Mlandizi), Zubeda Mgunda (Simba), Stumai Abdallah (JKT), Wema Richard (Mlandizi), Enekea Kasonga (Alliance), Vaileth Thadeo (Simba), Fatuma Issa (Evergreen), Vailet Singano (Simba), Happy Hezron (JKT), Janeth Christopher (Mlandizi) na Eva Wailes (Ruvuma).

Wengine ni Amina Ally (Simba), Diana Lucas (Ruvuma), Asha Hamza (Kigoma), Pheromena Daniel (Mlandizi), Opa Clement (Simba), Herieth Shija (Mash Academy), Donisia Minja(JKT), Joyce Fredy (Tanzanite), Janeth Shija (Simba), Masha Omari (Panama), Ester Mabanza (Alliance), Anastazia Nyandago (Panama), Rahabu Joshua (Alliance), Dotto Tosy (Simba) na Neema Charlse (Panama)

Wapo pia Lucia Mrema (Panama), Fumukazi Ally (JKT), Emeliana Mdimu (Makongo), Irene Kisisa (Kigoma ), Shamimu Ally (Ruvuma), Joyce Meshack (Makongo), Thadea Hamdan (Yanga), Rukia Hussein (Tanzanite), Aisha Masaka (Alliance), Agnes Palangyo (Tanzanite) na Angel Joseph wa Arusha.

Wakati Twiga Stars ikijifua kuna mataifa ambayo yana rekodi matata na tishio kwa timu za wanawake Afrika.

NIGERIA

Kikosi chao cha Super Falcon ni tishio barani humu kwani kina rekodi za kusisimua chini ya kocha wao Thomas Dennerbay na nahodha Desire Oparanoze.

Timu hiyo imewahi kushiriki michuano ya Fifa Womens World Cup na Africa Woman National Cup (Awcon) ambayo pia hutumika kufuzu michuano ya Kombe la Dunia ambapo kikosi hicho kimeshiriki mara 13 na kushinda mara 10 (1993, 1995, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2010, 2014 na 2016).

Mbali na hapo wamewahi kufika robo fainali mwaka 1999 wakiwa wameshiriki michuano hiyo mara nane.

Nigeria inangozwa na mlinda mlango Tochukwu Oluehi; mabeki ni Osinachi Ohale, Ngozi Ebere, Onome Ebi, Faith Michael, Chidinma Okeke ilhali viungo ni Amarachi Okoronkwo, Evelyn Nwabuokwu, Rita Chikwelu, Ngozi Okobi-Okeoghene, Halimatu Ayinde, Ogonna Chukwudi. Upande wa ushambuliaji yupo Anam Imo akiwa ndiye mshambuliaji muhimu na hatari akisaidiana na Asisat Oshora.

GHANA

Timu ya wanawake ya Ghana wanaojiita Black Queens chini ya kocha Mercy Tagoe Quarco na nahodha Elizabeth Addo, wana rekodi nzuri Afrika na bado wanafanya vizuri kwani wameshiriki michuano ya kimataifa mara nyingi ikiwemo Awcon mara 12 na kuwa washindi wa pili mara tatu (1998, 2002 na 2006).

Katika Kombe la Dunia la Wanawake hawako nyuma kwani wameshiriki mara tatu (1999, 2003 na 2007) na kuishia hatua ya kwanza.

Ghana ikiwa na Addo ambaye amepewa jukumu la unahodha, ndiye mchezaji wa kuangaliwa zaidi kwani rekodi yake ya kushiriki michuano mbalimbali ni ya kusisimua na amekuwa miongoni mwa nyota watatu waliowahi kutwaa tuzo kwenye michuano hiyo.

EQUATORIAL GUINEA

Kikosi hicho chini ya kocha Jean Paul Mpila, kina rekodi nzuri katika michuano mbalimbali. Timu hiyo imeshiriki michuano ya Awcon mara tano, imechukua ubingwa mara mbili (2000 na 2012). Mbali na michuano hiyo pia imeshiriki Kombe la Dunia kwa wanawake mara nane na mwaka 1999 waliingia 16 bora.

Equatorial Guinea wanaye mchezaji tegemeo, Genoveva Addo, ambaye amerikisa nyavu kwenye michuano mbalimbali ikiwemo Kombe la Dunia kwa wanawake akiwa amefunga 24 na ndiye nahodha wao.

Hivyo kwa timu kama Tanzania ambao si wazoefu sana wa michuano ya kimataifa wanatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha ili kuwa na mbinu mbalimbali kukabiliana nao.

AFRIKA KUSINI

Kikosi hiki ni miongoni mwa timu tishio barani Afrika kwani kimeshiriki michuano mbalimbali na kushika nafasi nzuri. Banyana Banyana imeshiriki michuano ya Awcon mara 12, imeshika nafasi ya pili mara sita (1995, 2000, 2002, 2008, 2012 na 2018). Mbali na hapo kikosi hicho kimeshiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa wanawake mara moja mwaka 2019 na kutolewa katika hatua za mwanzo. Afrika Kusini wenyewe wanatamba na nyota wao Janine Van Wyk ambaye anacheza nafasi ya beki na ndiye nahodha.

CAMEROON

Chini ya kocha Alain Djeurufa na nahodha wao, Christine Marie, wamekuwa miongoni mwa timu kali barani Afrika kwa upande wa wanawake.

Timu hiyo ina rekodi nzuri na bado wanaendelea kufanya vizuri katika michuano mbalimbali. Kikosi hicho kimeshiriki michuano ya Awcon mara 12 na kushika nafasi ya pili mwaka 1991, 2004, 2014 na 2016, hivyo ni rekodi nzuri kwao.

Mbali na michuano hiyo pia wameshiriki michezo ya Kombe la Dunia kwa wanawake mara mbili na kutinga 16 bora mwaka 2015 na 2019.

Hivyo Twiga Stars inapaswa kuendelea kujiweka fiti kwa ajili ya michuano mbalimbali inayoanza hivi karibuni kwani kuna timu za mataifa mengi zinazofanya vizuri kuliko wao. Kila la heri Twiga Stars.