Twanga Pepeta yawapa mzuka mashabiki Krismasi

Thursday December 27 2018

 

By Rhobi Chacha

Amekuambia nani dansi haiwezi kurudi mahala pake? Kama huamini we jaribu kutembelea katika kumbi zinazopiga muziki wa dansi usiku, utashuhudia nyomi la watu na hadi kufikia hatua ya kujiuliza wahusika wa dansi wamekosea wapi hadi wanashindwa kurudi kwa haraka katika chati.

Tukiachana na Onyesho la Sikinde na Msondo lililofanyika jana  pale TCC Club Chang’ombe na kuweza kujaza watu, hii imekuwa pia kwa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ nao walifunika kwa kujaza watu jana katika Ukumbi wa Jonzi Pub uliopo Magomeni Mikumi.

Wapenzi wa burudani walishuhudia onyesho la nguvu kutoka kwa  bendi hiyo na ilikuwa na ubunifu wa kipekee. Kwanza kuwachezesha mashabiki nyimbo moja baada ya nyingine, kuwachezesha wacheza shoo wao. Pili ni pale Charls Baba kuwachezesha wanamuziki mmoja mmoja kuanzia wapiga vyombo, waimbaji na wacheza shoo  wa bendi hiyo.

Kwa upande wa waimbaji walioimbishwa ni Luizer Mbutu, Fetty, Joshua, Kalala Junior na Charls Baba mwenyewe, huku wapiga vyombo ni Bright ambaye ni mpiga Tumba wa kike, Kirikuu mpiga Drum, wapiga gitaa ni Shaka Zulu, Lualua na Godfrey Kanuti.

Wacheza shoo ni Hamza Mapande ‘Mapande the boss’, Chiku, Maria Saloma na Stella Manyanya.

Mbali na hiyo, Meneja wa bendi hiyo, Martin Sospeter amesema mpiga gitaa Godfrey Kanuti amerudi kwenye bendi yake hiyo baada ya kuchomoka kwenda kutumikia bendi ya Mapacha Watatu Original ya Khalid Chokoraa.

Advertisement