Twaha Kiduku aletewa mbabe wa Tinampay

Baada ya kumaliza ubishi wa Tanzania ‘dabi’ Twaha Kassim ‘Kiduku’ sasa atawania mkanda wa WBC.

Bondia huyo atazichapa na Sirimongkhon Iamthuam ‘Sirimongkol Singwancha’ wa Thailand aliyewahi kumchapa Arnel Tinampay aliyewagawa mashabiki wa ndondi nchini kwenye pambano na Hassan Mwakinyo, Novemba, 2019.

Singwancha bondia namba moja nchini Thailand na wa 205 kati 1202 duniani kwenye uzani wa light heavy, ameshusha uzani ili kuzichapa na Kiduku Oktoba 30, jijini Dar es Salaam.

Hilo litakuwa pambano la kwanza la ubingwa wa WBC kupigwa nchini ambapo kwa mujibu wa Promota Shomari Kimbau litakuwa la raundi 12 la uzani wa super welter.

“Pambano litapigwa kwenye ukumbi wa PTA Sabasaba likitanguliwa na mapambno mengine sita,” alisema Kimbau.

Twaha licha ya kufanya vizuri katika ndondi nchini ikiwamo hivi karibuni kumchapa Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ katika pambano la ‘Tanzania dabi’, atakuwa na kibarua cha kumkabili Mthailand huyo mwenye uzoefu wa ndoa kwa miaka 26.

Singwancha, bondia wa nyota moja na nusu ana rekodi ya kushinda mapambano 97 (62 kwa KO), likiwamo na Tinampay, bondia aliyecheza na Mwakinyo jijini Dar es Salaam na kuonyesha upinzani, huku matokeo ya ushindi wa pointi kwa Mwakinyo yakiwagawa Watanzania.

Katika maisha yake ya ndondi, Mthailand huyo amepigwa mara nne (1 kwa KO), huku Twaha akiwa ameshinda mapambano 15 (manane kwa KO), amepigwa mara sita (moja kwa KO) na kutoka sare mara moja tangu 2013 alipoingia kwenye ngumi.

“Niko vizuri kama kawaida yangu, sina maneno mengi zaidi ya vitendo, Mthailand amejipendekeza lazima aumie,” alitamba Twaha aliyepo kambini mkoani Morogoro chini ya kocha Pawa Ilanda.

Bondia huyo namba mbili nchini kwenye uzani wa super welter mwenye nyota mbili na nusu, alisema yuko tayari kumkabiri Mthailand huyo na kubakisha ubingwa wa WBC nyumbani.