Twaha Kiduku: Kuna siku Mwakinyo ndiye ataomba pambano na mimi

Muktasari:

Twaha atazichapa na Sirimongkhon Iamthuam 'Sirimongkol Singwancha' wa Thailand pambano la raundi 10 la kuwania ubingwa wa WBC litakalopigwa kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba, Dar es Salaam

Twaha 'Kiduku' Kassim ametaja sababu za kutaka kuzichapa na Hassan Mwakinyo na kubainisha kwamba hakuomba pambano hilo ili liwapime nani ni zaidi ya mwenzake baina yao.

Amesema licha ya Mwakinyo kumgomea kuzichapa naye, lakini anaamini yeye Twaha atakapotwaa ubingwa wa WBC, Oktoba 30, kibao kitageuka na Mwakinyo ndiye atamuomba wapigane.

"Amenikatalia sasa, sawa nimekubali na lazima nikubali ili maisha mengine yaendelee, ndiyo sababu Oktoba 30 napigana na bondia kutoka nje ya Tanzania," alisema bondia huyo namba mbili nchini kwenye uzani wa super welter.

Alisema baada ya pambano hilo, hana shaka atapanda mara dufu kwenye viwango vya dunia na kipindi hicho Mwakinyo ndiye ataomba kupigana naye.

"Nikichukua ubingwa wa WBC, ambao naamini nitashinda, nitakuwa kwenye levo nyingine, nitapanda mara dufu kwenye ubora, uenda hata nikawa mimi ndiye namba moja, itakuwa ni zamu yake sasa kuomba kucheza na mimi," alisema.

Akizungumzia sababu za kumtaka Mwakinyo, bondia huyo alisema alifanya hivyo akiamini pambano lao lingekuwa na mvuto zaidi kwa mashabiki.

"Sikuwa na dhamira ya kutaka tuonyeshane nani ni zaidi ya mwenzake kwenye ngumi, la hasha, isipokuwa nilitaka tuwape ladha mashabiki wa ngumi ulingoni.

"Kwani mimi na nyota mbili na nusu sawa na Mwakinyo, rekodi zetu zinafafana, yeye ni namba moja na mimi namba mbili nchini kwenye uzani wa super welter.

"Hivyo pambano letu lingekuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki, tofauti na yeye angeletewa bondia kutoka nje ya nchi, lakini kwa kuwa amekataa, basi huwezikulazimisha jambo, lakini naamini nitakapochukua ubingwa wa WBC, yeye ndiye ataomba kupigana na mimi,"