Tuzo za CAF 2018: Vipengele vya kuwapata washindi vyatajwa

Muktasari:

Tuzo hizo zimekuwa zikitolewa tangu mwaka 2001, ambapo mshindi wa mwaka jana wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, alikuwa ni Mshambuliaji wa Misri na klabu ya Liverpool, Mohammed Salah.

Nairobi, Kenya. Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF), limetangaza vipengele 11 vitakavyotumika kumpata mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika, kwa mwaka wa 2018 (2018 CAF Awards).

Vipengele hivyo vilitolewa jana katika kikao cha kamati ya maandalizi ya tuzo hizo, iliyokutana Jijini Dakar, Senegal. Kwa mujibu wa kamati hiyo, tuzo hizo zimepangwa kufanyika Jumanne ya Januari 8, 2019.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyochapishwa kwenye mtandao wa CAF, safari hii, mbali na tuzo zingine zilizozoeleka, kutakuwa na tuzo maalum kwa ajili ya maafisa na wasimamizi wa masuala ya uendeshaji wa soka, pamoja na tuzo ya kikosi bora cha mwaka (best eleven).

Ni kwamba, mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa kiume na mwanasoka bora wa kike, atapatikana kwa kupigiwa kura na kamati ya ufundi na maendeleo ya CAF, wanahabari wa michezo, wanasoka wa zamani, makocha na manahodha kutoka vilabu 54wanachama wa CAF.

Vipengele hivyo:

Mwanasoka bora wa mwaka (wanaume na wanawake), Mchezaji bora chipukizi, Kocha Bora wa mwaka (wanaume na wanawake), Timu bora ya taifa (wanaume na wanawake), goli bora la mwaka.

Pia kutakuwa na tuzo kikosi bora cha mwaka (Best XI), tuzo ya rais bora wa shirikisho la soka (Ydnekatchew Tessema Trophy for the Federation President of the Year), na tuzo ya Heshima (Platinum Award)