Tuyisenge ameamsha dude Gor Mahia

Thursday August 9 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Kipigo cha kwanza katika ligi msimu huu walichokipata Gor Mahia mbele ya Bandari wala siyo habari ya mjini. Kuondoka kwa Meddie Kagere pia sio habari ya mjini tena. Habari kuu ni goli alilofunga  Mnyarwanda Jacques Tuyisenge.
Licha ya kufungwa 2-1 na Bandari huko Mbaraki, Mombasa, bao alilolifunga fowadi huyo liliamsha dude kwenye ligi sio kidogo.
Ndio, Tuyisenge alifunga bao lake la 12 na hivyo kuongeza ushindani kwenye mbio za mfungaji bora akiwa nyuma ya Kinara, Elvis Rupia, kwa mabao matatu tu.
Mpaka sasa, Rupia aliyetimkia Ligi Kuu ya nchini Zambia, ndiye anayeongoza akiwa na mabao 15 na kuondoka kwake kunamaanisha mbio za kuwania kiatu cha dhahahu kipo kati ya Whyvonne Isuza (AFC Leopards), Nicholas Kipkirui na Mike Madoya (Zoo Kericho).
Hata hivyo; kati ya wanne hao, ni Tuyisenge anayeonekana kuwa na ubavu wa kuondoka na kiatu hicho, hasa kutokana na Gor Mahia kuwa na mechi nyingi (mechi tatu mkononi), mpinzani wake wa karibu ambaye ni Isuza (11), kufungiwa mechi mbili huku Kipkirui (11) na Madoya (10) kuonekana kuishiwa makali ya kutupia kambani.
Vinara wa kutupia Kambani:
15. Elvis Rupia (Nzoia Sugar)
12. Jacques Tuyisenge (Gor Mahia)
11. Yvonne Isuza (Leopards)
Nicholas Kipkirui (Zoo)
10. Michael Madoya (Zoo)
 Cliff Alwanga (Mathare)
9. Ezekiel Odera (Leopards)
Cliff Nyakeya (Mathare)
8. Ephrem Guikam (Gor Mahia)
 Timothy Otieno (Tusker)

Advertisement