Tusitarajie maajabu yoyote Kariakoo Derby

Sunday September 30 2018

 

HUKO mitaani kumekuwa na kelele nyingi, kisa pambano la watani wa jadi , Simba na Yanga. Hata asubuhi hii mitaa mbalimbali ya jiji la Dar na vitongoji vyake kuna vurugu kwa ajili ya shamrashamra za mpambano huo.

Kuna baadhi ya majina yanatajwa sana...Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu na wengine, wakitabiriwa kumaliza mechi mapema.

Wapo walioamua kubeti mapema kwa kutabiri nani atakayeibuka na ushindi kwa kuangalia tu aina ya vikosi walivyonavyo.

Ila kwa uzoefu wa mechi za watani, naamini kabisa hakutana na kipya ama cha ajabu katika pambano hilo, zaidi ya burudani ya mchezaji mmoja mmoja.

Bato ya Cletus Chama dhidi ya Fei Toto itaburudisha, Kagere na Yondani ama Dante na Okwi itanoga kama itakavyokuwa vita ya Makambo na Nyoni ama Ajibu na Wawa.

Kwa aina ya vikosi na mifumo inayotumiwa na makocha wa timu hizo watakaokutana kwa mara ya kwanza katika dabi, utamu utakuwa katikati na pembeni.

Ila kama unatarajia kiu ya muda mrefu ya kushuhudia hat trick nyingine katika dabi sahau kwa mchezo wa leo. Hili naweza kubeti kwani, sioni kama Makambo, Ajibu, Tambwe ama Kagere, Okwi ama Kichuya kama wanaweza kuvunja rekodi ya King Kibadeni aliyoiweka miaka 41 iliyopita. Ni kweli nyota hao wanafunga, lakini linapokuja pambano la watani lenye mambo mengi ndani na nje ya uwanja nashindwa kuona wa kuivunja rekodi ya King. Ndio maana wamekuja na kuondoka nyota kibao wakiigwaya!

Kinachoweza kuwa gumzo, labda ni kadi nyekundu inayoweza kutolewa na refa Jonesia Rukyaa kwa wachezaji watukutu watakaojichanganya mbele yake. Jonesia hana utani. Vinginevyo tusubiri tu kushuhudia dakika 90 zikiisha kila mmoja akitoa lawama na mwishowe labda kuwa mwisho wa Masoud Djuma kuwa ndani ya kikosi cha Msimbazi, ila chondechonde msininukuu wala msiende kubeti, mtaliwa!

Advertisement