Tunda Man: Morrison Simba hapamfai

Muktasari:

Japokuwa mchezaji huyo amekuwa na kiwango na uwezo mzuri, lakini utovu wa nidhamu umekuwa mtihani mkubwa sana kwake

UONGOZI wa Simba umeshauriwa kuwa makini kama wanamuhitaji mchezaji wa Yanga, Bernard Morrison kutokana na utovu wake wa nidhamu ambao sio taswira nzuri katika soka na maendeleo yake kwa ujumla.

Morrison amekuwa kwenye mgogoro na viongozi wake huku akionyesha utovu wa nidhamu wa waziwazi mara kwa mara, licha ya kuchukuliwa hatua kwa kukatwa mshahara wake hivi karibuni, lakini amekuwa akishindwa kubadilika.

Nyota huyo wakati timu yake ikijiandaa na mchezo dhidi ya Mwadui uliopigwa juzi na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 alionekana akiwa katika michezo ya mtaani (Ndondo) huku akishindwa kutokea mazoezini.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Tunda Man aliyeweka ahadi ya kuchoma gari yake aina ya Toyota Mark X DBJ 616 endapo wangefungwa na Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Katika mechi hiyo, Simba iliibuka na ushindi wa bao 4-1 ambao uliwafanya watinge fainali za mashindano hayo ambapo watacheza na Namungo, Agosti 2 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Tunda Man amesema kama Simba wanamuhitaji wanatakiwa kutafakari sana na kuangalia alichowafanyia watani zao, kwani anaweza kukifanya tena kwao, hivyo licha ya ubora wake ndani ya uwanja bila ya nidhamu ni kazi bure.

"Mchezo wa mpira ni kazi kama kazi nyingine, lakini nashangaa sana Morrison ni mchezaji mzuri ila sijui ana shida gani, kama kweli viongozi wangu wanamuhitaji inabidi wakubaliane juu ya tabia zake za ajabu,"

"Mimi ni Simba damu, lakini kitendo cha mchezaji huyu kuonyesha utovu wa nidhamu kwa viongozi na wachezaji wenzake na jamii kwa ujumla kinanikera na hata sipendezewi kabisa, hivyo wachezaji wako wengi tu,"

"Mtu kama anashindwa kuheshimu kazi yake inayomfanya kupata chakula si hatari sana hiyo, maana siku ya mchezo wetu na wao Yanga alitolewa akaondoka moja kwa moja kwenda vyumbani, ni nidhamu mbovu sana, kwani hata Ronaldo na Mess na ustaa wao wanatolewa uwanjani wanaenda benchi,"

Wakati huo huo, Tunda Man amesema mipango yake ya kutangaza kuchoma gari lake endapo wangefungwa na Yanga katika mchezo huo amedai ilikuwepo lakini aliweka kipaumbele kwanza dini na Serikali kabla ya kufanya maamuzi hayo endapo angefungwa.

"Mimi ni Muislamu buana nafuata sana dini, pia Serikali kama sheria isingeniruhusu kufanya hivyo nisingeweza kufanya, ningetafuta njia mbadala ambayo ningeweza kulipeleka hata kwa watoto yatima wakauza pesa ikawasaidia kwa namna yoyote ile,"