Tunawasubiri Algeria, Mtajua kutufahamu Gor Mahia

Thursday February 28 2019

 

Algiers, Algeria. Timu ya Hussein Dey ya Algeria imewaambia Gor Mahia watapata wakati mgumu katika mchezo wao wa Jumapili wa Kombe la Shirikisho Afrika CAF.

Miamba hiyo ya Kenya ilichakaza timu hiyo ya Afrika Kaskazini kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Nairobi.

Hussein Dey ililalamika kuhusu kupata mapokezi mabaya kutoka wenyeji mabingwa wa Kenya na tayari kupitia mitandao ya kijamii wameweka bayana kuwa Gor Mahia itakuwa katika wakati mgumu Algiers.

"Hili ni deni. Wakati mtakapokuja Algeria mtatujua vizuri. Gor Mahia walishindwa kutuandalia basi na mazoezi wametupeleka kwenye uwanja wa kriketi. Wakati wa mchezo walikuwa wakirusha vitu uwanjani," ilisema moja ya ujumbe wao.

Tayari klabu hiyo imeanza kuwahamasisha mashabiki wao kutokea kwa wingi katika uwanja wa Sted Juillet 1962 mjini Algiers ambao ndio wamewatengea Gor kutumia   kufanyia mazoezi yao.

Kwa mujibu wa sheria za CAF, kwenye mechi za nyumbani, mwenyeji  anatakiwa kutoa usafiri na uwanja mzuri wa mazoezi kwa mpinzani wake.

Advertisement