Tunaishi katika wakati mzuri sana kisoka

Muktasari:

Tumeona madada na mabinti zetu wa Tanzanite wakifanya maajabu kwa kutwaa Kombe la Cosafa wiki iliyopita. Hatujawahi kutwaa kombe hilo kwa wanawake tangu tuwe taifa baada ya Uhuru na haya hayawezi kuwa mafanikio ya kawaida.

FUMBA macho halafu waza mambo machache yafuatayo; Tanzania ina mchezaji katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, ina wachezaji walau dazeni moja wanaocheza katika klabu mbalimbali nje ya nchi na ndiyo kwanza imetoka kushiriki katika Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

Mechi za klabu zake kubwa zinazochezwa katika Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kujaza watu takribani 60,000 zinajaza watu kiasi kwamba, taifa letu sasa limekuwa hadithi inayozungumzwa na nchi majirani.

Timu zetu za Taifa; kuanzia za vijana, wakubwa na hata wanawake sio tu kwamba zinashiriki katika mashindano mbalimbali kila uchao–bali sasa zimeanza kupiga hatua moja zaidi ya kushinda mashindano.

Tumeona madada na mabinti zetu wa Tanzanite wakifanya maajabu kwa kutwaa Kombe la Cosafa wiki iliyopita. Hatujawahi kutwaa kombe hilo kwa wanawake tangu tuwe taifa baada ya Uhuru na haya hayawezi kuwa mafanikio ya kawaida.

Kwa mwenendo huu, kama utaendelea kama tunavyotaraji, naanza kuhisi miaka mingi ijayo, watakaokuja wanaweza kuona pengine sisi tunaoshuhudia mambo haya sasa tuliishi katika kizazi cha dhahabu katika mchezo wa soka.

Klabu ya Simba inaelekea katika mabadiliko makubwa ya kimfumo na kama tukiamua kuzungumza Kiswahili cha mpirani, unaweza kabisa kusema gari limeshawaka.

Unaona hivyo hivyo kwa Yanga chini ya uongozi wa Dk Mshindo Msolla na Frederick Mwakalebela. Na kwa sababu Watanzania tunafahamika kwa tabia za kuiga yaliyo mazuri kwa wenzetu, nadhani muda si muda mrefu wengine nao wataelekea huko huko.

Nisisahau kusema mechi zote za Ligi Kuu ya Tanzania na mashindano mengine yanayoendeshwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaonyeshwa kupitia televisheni.

Pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania, Watanzania sasa wanatazama zaidi ligi yao kuliko huko nyuma. Zamani ilimpasa mtu kwenda mpirani kuifahamu klabu, leo hii wapo watu ambao hawajawahi kukanyaga viwanjani, lakini wanawajua wachezaji na wanatazama mipira wakiwa sebuleni au kwenye kumbi.

Nimesafiri katika nchi nyingi za Afrika na naamini naweza kuwa mtu mzuri kusema kwamba, Tanzania kisoka sasa inaelekea kuwa mojawapo ya nchi kubwa barani Afrika hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Inawezekana kabisa Wakenya na Waganda wana wachezaji wengi zaidi nje, lakini hiyo ni athari ya miaka takribani 10 iliyopita. Kama Tanzania itaendelea katika njia hii inayopita sasa, sina shaka tutakuwa na wachezaji wengi kuliko Kenya na Uganda nje ya nchi.

Kama wachezaji kama Eliud Ambokile na Ramadhani Singano wameweza kuonwa na timu kubwa kama TP Mazembe, nina uhakika kizazi cha akina Kelvin John ‘Mbappe’ kinaweza kusogea mbali zaidi.

La msingi ni kwa TFF na viongozi wa klabu kuendelea kufanya mambo makubwa na mazuri ambayo wanaendelea nayo kwa muda huu. Kuhakikisha mashindano mbalimbali yanaendelea na timu zetu kushiriki, kukuza hamasa kwa mashabiki na wadhamini na kuboresha miundombinu ya kisoka; ikiwamo kuleta wataalamu zaidi, kufundisha zaidi watu wetu na kutengeneza mazingira mazuri kwa vipaji vilivyopo kuonekana na kupata nafasi ya kuvionyesha.

Labda hatuoni kwa sababu wengine macho yetu yamekaa kukosoa zaidi (ambayo si tabia mbaya kwa sababu inasaidia watu wasibweteke), lakini ukweli ni kwamba kuna vitu vinakwenda vizuri na tunapaswa pia kulitambua hilo.

Mshairi maarufu hapa nchini, Amri Sudi Andanenga, ambaye ni mlemavu wa macho aliwahi kulalama huko nyuma kwamba kipofu na asiyeona ni watu wawili tofauti; kwamba kipofu ni mlemavu wa macho (kama alivyo yeye) lakini anaweza kabisa kuwa anaona vizuri kuliko hata wale wenye macho, lakini hawaoni mambo vizuri.

Yawezekana kabisa wengi wetu tuna macho mazima kabisa lakini, tumekosa fursa ya kuona kwamba pengine sisi tunaishi katika wakati bora zaidi kisoka kwa taifa letu. Nadhani iko siku kuna watu wataona.