Tulieni,Pogba anaibukia Etihad

Muktasari:

Pogba alipata maumivu ya enka na kumfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

MANCHESTER, ENGLAND . MANCHESTER United imepata matumaini huenda wakawa na huduma ya kiungo wao, Paul Pogba kwenye mchezo wa Manchester derby utakaopigwa zaidi ya wiki tatu zijazo kutoka sasa.

Kiungo huyo Mfaransa amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu kwenye mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Arsenal iliyopigwa Old Trafford Septemba.

Pogba alipata maumivu ya enka na kumfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Lakini siku za karibuni ameonekana huko mazoezini Carrington kitu kinachowapa matumaini Man United kwamba huenda wakawa na huduma yake katika mechi ya kuwakabili Manchester City itakayopigwa Etihad, Desemba 7.

Jumanne ijayo, staa huyo anatazamiwa kuanza rasmi mazoezi ya mpira na atakuwa kwenye kikosi cha watoto kwa muda kabla ya kurudi kwenye kasi yake na kurejea katika chama la Kocha Ole Gunnar Solskjaer, ambalo hakika limemisi sana huduma yake kwa muda mrefu.

Taarifa ya ndani ya Man United ilifichua: “Ole anataka awepo kwenye benchi katika mechi hiyo kama ikiwezekana. Amekuwa akijiweka fiti katika suala la ari na ukweli siku zote amekuwa mchezaji wa kiwango cha juu.” Pogba alituma video kwenye ukurasa wake wa Instagram Jumatatu iliyopita ikionyesha akiondolewa bandeji kwenye mguu wake, hivyo ikiwa ni dalili nzuri kwamba amepona na si muda mrefu mashabiki wa Man United wataanza kumwona uwanjani akiwa ndani ya jezi yao.

Wakati huohuo, Man United imethibitisha kiungo wao Scott McTominay amejiondoa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Scotland kwa ajili ya mechi zijazo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya enka. Jambo hilo linamfanya Kocha Ole kuamini hadi kufikia Desemba 7, kiungo huyo atakuwa fiti kwenye kupiga mzigo Etihad. Manch United iko katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 16.