Tulieni, Serengeti Boys itafuzu tu

Muktasari:

  • Waziri alisema ana uhakika mechi ijayo Serengeti Boys itashinda na kuwaomba Watanzania wote wajitokeze kwa wingi kushuhudia mashindano haya kwani hakuna tena viingilio na wanatakiwa kuonyesha kweli haya mashindano hayajakosewa kuletwa Tanzania.

ACHANA na matokeo ya kipigo walichokipata Serengeti Boys kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Nigeria cha mabao 5-4, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema vijana wake wana nafasi ya kufuzu kwenda Kombe la Dunia.

Mwakyembe alisema Serengeti Boys inayoshiriki michuano ya AFCON kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 sio timu dhaifu ina uwezo wa kushinda mechi mbili zilizobaki dhidi ya Uganda na Angola ambazo ndizo zilizoshikiria tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia.

“Nadhani wenzetu waliingia kwa kujiamini kwani Nigeria ni wazoefu kwenye soka, lakini vile vile vijana wengi wanacheza timu za vijana nje ya Afrika wakati vijana wetu wote wanacheza timu za hapa ndani,” alisema.

Alisema kwa mpira ulioonyeshwa ni kweli Tanzania ipo ulimwengu wa soka kwa kumaliza dakika 90 na timu kama Nigeria ikiwa na matokeo hayo.

“Vijana wetu wamejitahidi sana katika kundi letu tutacheza mechi mbili zilizobaki na kwa soka waliloonyesha Serengeti Boys hakika tuna nafasi ya kushinda mechi zote zilizobaki.

“Hizi motisha ambazo wanapewa au wameahidiwa wachezaji wa Serengeti Boys sidhani kama zina nafasi kwa wakati huu kinachotakiwa ni kuweka uzalendo mbele ili kuhakikisha mechi mbili zilizobaki tunashinda na kupata nafasi ya kwenda kombe la dunia,” alisema na kuongeza;

“Kiukweli sasa hivi Tanzania kisoka tumeendelea na kama tungecheza na timu nyingine ya kawaida si bora kama Nigeria tulikuwa tuna uwezo wa kuwafunga zaidi ya mabao tisa, kwani tumeonyesha soka zuri na la hali ya juu, nafikiri hata wapinzani walishangazwa sana kwa hilo.

Waziri alisema ana uhakika mechi ijayo Serengeti Boys itashinda na kuwaomba Watanzania wote wajitokeze kwa wingi kushuhudia mashindano haya kwani hakuna tena viingilio na wanatakiwa kuonyesha kweli haya mashindano hayajakosewa kuletwa Tanzania.

Mara baada ya mechi yao ya kesho Serengeti itarudi tena Uwanja wa Apri 20 kwa kumalizana na Angola.

Timu nne, mbili kutoka kila kundi zitafuzu nusu fainali, lakini pia zitakata tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia za Vijanja zitakazofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Brazili.