Tukutane kwa Mchina

Muktasari:

  • Feisal Salum aliyeanza mchezo huo sambamba na Papy Kabamba Tshishimbi, aliwanyanyua mashabiki wa Yanga waliojazana uwanjani kwa kufunga bao hilo muhimu na la pekee akirejea alichokifanya kwenye mechi mchezo dhidi ya KMC iliyopigwa Oktoba 25 mwaka jana.

JANGWANI kumenoga. Mizuka imepanda kwa mashabiki wa Yanga kiasi cha kupata nguvu za kuwatambia watano zao. Unajua nini? Baada ya kucheza kwa muda wa dakika 270 bila kupata ushindi kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga jana Jumapili ilipata ushindi wao wa kwanza kwa kuinyuka JKT Tanzania, huku mashabiki wao wakiimba ‘Kama vipi.

Tukutane kwa Mchina...’ Wakimaanisha kuwaambia watani zao Simba kuwa, wakutane Uwanja wa Taifa ambako wikiendi hii watavaana kwenye mchezo wa marudiano baina yao, ili kumaliza tambo.

Simba yenyewe kesho Jumanne itakuwa kwenye mtihani wa mechi za kimataifa kwa kuvaana na Al Ahly ya Misri ambao wiki iliyopita waliwafumua mabao 5-0 mjini Alexandria, Misri.

Katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu, Vijana wa Mwinyi Zahera walijikuta wakipoteza alama saba kwa kufungwa na Stand United bao 1-0 kisha kulazimishwa sare ya 1-1 na Coastal Union kabla ya Jumatano kubanwa tena na Singida United kwa kutoka suluhu mjini Singida.

Lakini jana wakicheza huku wakiwa na uchovu na wakiwakosa baadhi ya nyota wao akiwamo, straika Heritier Makambo, Thabani Kamusoko na kuanzishwa benchi kwa Kelvin Yondani, Yanga ilionyesha kuzinduka kwa kuwakimbiza wenyeji wao na kuwachapa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Feisal Salum aliyeanza mchezo huo sambamba na Papy Kabamba Tshishimbi, aliwanyanyua mashabiki wa Yanga waliojazana uwanjani kwa kufunga bao hilo muhimu na la pekee akirejea alichokifanya kwenye mechi mchezo dhidi ya KMC iliyopigwa Oktoba 25 mwaka jana.

Kiungo huyo alifunga bao hilo baada ya kumalizia krosi pasi murua ya beki Gadiel Michael katika dakika ya 27 lililowasumbua wenyeji wao kulirejesha licha ya kufanya mashabulizi mengi katika kila kipindi na kumpa wakati mgumu kipa Ramadhani Kabwili na mabeki wake.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha alama 58 baada ya mechi 23, ikiiacha Azam iliyopo nafasi ya pili kwa alama 10 na pointi 22 dhidi ya Simba, KMC na Lipuli ambazo kila moja ina alama 36 licha ya kutofautiana idadi ya michezo iliyocheza mpaka sasa katika ligi hiyo.

Bao hilo la Fei Toto ni la nne kwake tangu atua Jangwani msimu huu akitokea JKU ya Zanzibar na lilipokelewa kwa bashasha kubwa na mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa wakiimba kuwatania watani zao wa Simba itakovaana nao Jumamosi hii katika mechi tya marudiano.

Kabla ya mchezo huo Yanga ilirejea tukio ililolifanya ilipocheza na Coastala kwenye uwanja huo kwa kugomea kuingia vyumba vya kubadilishia nguo, huku wakimtambuliza Tshishimbi kutangulia kushuka kutoka kwenye basi lao walipowasili uwanjani.

Kipindi cha pili Yanga ilimpumzisha Mrisho Ngassa na kuingia Mohammed Issa ‘MO Banka’ aliyekuwa akishuka uwanjani kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe, baada ya kumaliza adhabu yake ya miezi 14 kwa kosa la kutumia bangi.

Pia Yanga ilimtoa nahodha Ibrahim Ajibu na kuingiza Deus Kaseke, kisha Buswita na kumuingiza Yondani, huku JKT ikimtoa Samwel Kamuntu na kuingia Said Luyaya mabadiliko ambayo hata hivyo halikubadilisha chochote mpaka dakika 90 zilipopulizwa na mwamuzi, Elly Sasii.

Mara baada ya mchezo huo, Yanga ilikuwa inaanza safari ya kuelekea Morogoro kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wao na Simba, huku Kocha wake, Mwinyi Zahera akisisitiza kuwa, ratiba ya sasa inawapa wakati mgumu vijana wake, japo wanapambana kibishi.

Katika mechi nyingine, KMC ilishindwa kutamba nyumbani kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Alliance. Wenyeji walianza kuandika bao dakika ya 50 kupitia Abdul Hilal kabla ya Alliance kuchomoa dakika ya 64 lililofungwa na Israel Patrick.