Tshishimbi awavuruga Yanga

Thursday March 26 2020

 

By CLEZENCIA TRYPHONE

UPEPO Jangwani ghafla umebadilika. Achana na ishu ya kampuni ya GSM kuandika barua ya kutaka kusitisha kutoa huduma walizokuwa wakizitoa nje ya mkataba, ila unaambiwa kiungo fundi wa timu hiyo, Papy Kabamba Tshishimbi amelianzisha huko huku Simba ikitajwa.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, mabosi wa klabu hiyo wamevurugwa baada ya kusikia kiungo huyo anahusishwa na dili la kutua Msimbazi na baadhi yao kumwakia hivyo kashindwa kuvumilia na kufunguka ishu nzima za usajili wake.

Mkataba wa Tshishimbi imebakiza miezi minne kumalizika na tayari mazungumzo ya awali na viongozi wa Yanga kumuongezea yameshafanyika, lakini inadaiwa Simba wanafanya mchakato kimya kimya kumshusha Msimbazi.

Kibaya zaidi, amekaririwa akihojiwa kwenye kituo kimoja cha redio juu ya ishu hiyo nzima, na hilo ndilo lililowatibua mabosi wake na kumwakia wakiona kama anataka kuwasaliti kitu kilichomfanya naye kuwajia juu na kueleza ukweli wote.

Ipo hivi. Inadaiwa kuwa hatua ya kiungo huyo ambaye ndiye nahodha wa Yanga, kuzungumza na Simba na vyombo vya habari kimewakera na jana wakamuweka kikao jambo ambalo ameonekana kuchukizwa nalo akidai wamemuona kama mtoto wakati anajitambua.

“Tshishimbi katutibua sana, ni mchezaji tunayemtegemea na kazi yake tunaihitaji, lakini kitendo cha kuzungumza na Simba na vyombo vya habari wakati sio taratibu za kazi kimetukera japo ana haki ya kufanya hivyo,” kilisema chanzo kutoka uongozi wa Yanga aliyekataa kuandikwa jina lake gazetini.

Advertisement

Mtoa habari huyo alikiri kuwa mkataba wa Mkongo huyo uko ukingoni na kuwa ni moja ya wachezaji ambaye alitakiwa kukaa mezani na viongozi kujadili, lakini inaonekana dau la Simba limemchanganya na hapo ndipo tatizo linapoanzia.

“Ndio, tunajua Simba hawashindwi kwani wako vizuri kwa udhamini walionao huku Yanga mara unasikia GSM kasusa mara nini ni mtihani kidogo, lakini Pappy alipaswa kuzungumza nasi na sio alivyofanya na mkataba ndio shida,” alisema.

Alisema kuwa wanaamini Simba wana hasira kwa kumkosa Bernard Morrison na sasa wamehamia kwa Tshishimbi, kitu alichosema hawapo tayari kuona kikitokea, lakini wanamlaumu nyota huyo kutowajulisha.

Inaelezwa kuwa Simba wanawania saini ya Tshishimbi ili kuziba nafasi ya Mbrazil, Gerson Fraga atakayefungashiwa virago.

Tshishimbi alisajiliwa na Yanga mwaka Januari, 2018 akitokea Mbabane Swallows ya e-Swatin na mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Simba katika Kombe la Mapinduzi na kuupiga mpira mwingi ambao, uliwavuruga mabosi wa Simba na tangu wakati huo wamekuwa wakimfuatilia bila mafanikio.

MSIKIE TSHISHIMBI

Akizungumza na Mwanaspoti Tshishimbi amekiri kupigiwa simu na bosi mmoja ndani ya Yanga na kumtumia meseji ambazo binafsi hazikumfurahisha.

“Wengi wamenipigia simu, hata sijui wengine ni viongozi au la, ila nikikumbuka majina nitasema, mara ananiuliza Mwakalebela (Fredrick-Makamu mwenyekiti wa Yanga) alikutumia ujumbe kwa whatsapp, nikashangaa ina maana hana salio la kunipigia, mara sijui kwa nini naongea na vyombo vya habari, wakati hata ni mambo binafsi na hayahusiani na ishu ya mkataba wangu,” alisema.

Alisema simu na meseji zote zilimtaka aende ofisini jana asubuhi, lakini hakwenda kwa sababu ya kuzingatia agizo la serikali la kutaka wakae majumbani kipindi hiki cha corona.

“ Klabu ina mambo mengi, hata kama nimeongea na Simba kuna namna ya kuniita na sio utaratibu wa kupigwa simu wakati mwingine usiku na kufokewa kama mtoto ama kunidhalilisha. Najua mimi bado ni mchezaji wa Yanga hata kama mkataba wangu uko mwishoni, ila sipendi dharau hasa katika kazi yangu ya soka,” alisema.

Advertisement