Tshishimbi awafuata Ngoma, Chirwa Azam

Muktasari:

  • KIUNGO wa Yanga Papy Kabamba Tshishimbi amenaswa katika rada za Azam ambao walitamba kuwa na uwezo wa kumsajili kama walivyofanya kwa Obrey Chirwa.
  • Kocha wa Azam Hans Van Pluijm aliweka wazi kuwa Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji wazuri waliokuwa katika Ligi Kuu Bara.

WAKATI dirisha dogo la usajili kilifunguliwa rasmi leo Alhamisi, huku Azam mambo hayapoi kwani inaelezwa kiungo mahiri wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi naye yupo njiani ili kuwafuata kina Obtey Chirwa na Donald Ngoma.

Chirwa amenaswa na Azam hivi karibuni, baada ya Yanga kudengua kumrejesha kikosini akitokea Misri na kumfanya aungane na Ngoma waliowahi kucheza pamoja tangu wakiwa Zimbabwe kabla ya kukutana Yanga misimu miwili iliyopita. Hata hivyo ni wazi Kocha Hans Pluijm amelipania taji la Ligi Kuu Bara baada ya kuelezwa kwa sasa anapiga hesabu za kumbeba Tshishimbi anayemaliza mkataba wake Jangwani.

Inaelezwa kuwa Azam kwa sasa imeanza kufanya mchakato wa kusajili Tshishimbi kutokana na maelekezo ya kocha wao, Hans Pluijm.

Meneja wa Azam, Philip Alando alisema kuwa, wao wanafanya kazi ya usajili kwa kufuata maelekezo ambayo wanapewa na kocha wao juu ya mchezaji gani anayemhitaji naye watampa. hata awe nani mradi wana uwezo wa kumpata. Alando alisema baada ya kumalizana na Chirwa akili zao kwa sasa zipo kwa Tshishimbi, japo hakuweza wazi kama kocha Pluijm amemtaka, ila alizuga kwa kusema iwapo kama kocha wao atawaletea ombi la kumtaka Tshishimbi watahakikisha wanamsajili, kwani lengo lao ni kuona Azam inabeba tena taji.

“Maneno yamekuwa mengi mno mara baada ya kumsajili Chirwa, lakini baada ya kumalizana naye kwa sasa tunayemwangalia ni Tshishimbi na kama kocha atakuwa na mahitaji naye tuna uwezo wa kumsajili,” alisema Alando.

Naye Kocha wa Azam, Pluijm alisema Tshishimbi ni mchezaji mzuri aliokuwa katika ligi na kama kutakuwa na mpango wowote wa usajili hilo sio jukumu lake bali ni kazi ya uongozi.