Tshishimbi atuma salamu Rollers

Muktasari:

Naye Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema ushindi dhidi ya Rollers upo pale pale kwani, maandalizi aliyoyafanya kwa wachezaji wake katika Ukanda wa Kaskazini lengo ni kwenda kuimaliza Rollers.


USHINDI wa bao 1-0 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya AFC Leopard ya Kenya, umempa mzuka kiungo, Papy Kabamba Tshishimbi na sasa ameonya wanakwenda kumaliza kazi kwa Township Rollers.

Yanga ilikuwa Arusha kwa kambi ya siku tatu kuakisi hali ya hewa ya ubaridi ya mkoani hapa ambayo ni sawia na ile ya Botswana na kucheza mechi dhidi ya AFC Leopard.

Mchezo huo uliopigwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Yanga iliibuka na ushindi huo huku Tshishimbi akipiga bao safi na kuwapa shangwe mashabiki akimalizia mpira wa kona wa Patrick Sibomana.

“Tumepata nguvu mpya, lakini ushindi huu hautakuwa na maana kama hatutashinda dhidi ya Rollers kwani, lengo la mechi na AFC ni kuongeza morali ya kwenda kufanya kweli kule Botswana,” alisema Tshishimbi.

Naye Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema ushindi dhidi ya Rollers upo pale pale kwani, maandalizi aliyoyafanya kwa wachezaji wake katika Ukanda wa Kaskazini lengo ni kwenda kuimaliza Rollers.

“Maandalizi yapo vizuri lakini haikuwa kipimo kizuri kuwapima wachezaji wanaokwenda kucheza dhidi ya Rollers,” alisema.