Tshishimbi atoroshwa usiku Simba

Friday March 15 2019

 

By KHATIMU NAHEKA

WAMESHTUKA buana! Mabosi wa Yanga usiku mnene wamekutana na nyota wao wote kabla ya kuondoka kuifuata Lipuli ya Iringa kama njia ya kuwekana sawa, kisha wakawajaza mamilioni flani ya fedha kisha wakamshika mkono kiungo wa Papy Kabamba Tshishimbi wakimtaarifu, sasa wanaingia rasmi katika mazungumzo ya mkataba mpya klabuni hapo.

Kikao hicho kilichofanyika juzi Jumatano katika hoteli inayotumiwa na timu hiyo ya Nefaland iliyopo Manzese Argentina, vigogo wanaofanya kazi katika masuala ya usajili wakiongozwa na Mwenyekiti wao Hussein Nyika walimwita Tshishimbi na kufanya kikao kifupi cha faragha.

Katika kikao hicho, bosi mmoja amevujisha kiungo huyo ambaye anahusishwa pia kutakiwa na Simba alipewa kazi ya kujiandaa na mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na mkataba wake wa sasa unafikia ukingoni mwisho wa msimu huu.

Mazungumzo hayo yataanza haraka mara baada ya timu hiyo kurejea kutoka Iringa na kiungo huyo raia wa DR Congo atakutana na mabosi hao, lengo likiwa kumzuia asiende Msimbazi.

Mbali na mazungumzo hayo ya kuongeza mkataba mabosi hao walimpongeza kiungo huyo katika kiwango chake cha sasa wakimwambia sasa amerejea Tshishimbi waliyekuwa wanamjua.

Baada ya kikao hicho Mwanaspoti lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Nyika ambaye alifafanua kikao hicho ni cha kawaida kwao kukutana na wachezaji wao.

Nyika alisema Tshishimbi ni mmoja wa wachezaji wao muhimu na licha ya kuwa bado ana mkataba lakini suala la kubakia kwao sio kitu kipya kwa kuwa hawajahi kutamka wanataka kumwacha.

“Tshishimbi ni kijana wetu yuko hapa na ana mkataba halali, tulikuwa tunapanga naye mikakati ya sasa na baadaye kwa kuwa ni mmoja wa watu tunaowahitaji zaidi,” alisema Nyika.

“Tunafurahi sasa yuko katika kiwango bora baada ya kupona majeraha yake na unaposema tunataka kumuongeza mkataba Yanga hatujawahi kutamka labda tunataka kumwacha tuna imani naye ndiyo maana yupo hapa sana.”

MASTA WAJAZWA MAMILIONI

Katika kikao hicho mabosi hao katika kuwajaza upepo vijana wao kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Lipuli wakawajaza mamilioni kuhakikisha wanakuwa na hamasa kubwa.

Yanga itakuwa wageni wa Lipuli kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, huku wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa awali jijini Dar kwa bao 1-0.

Wakiongozwa na Kaimu Mwenyekiti, Samuel Lukumay mabosi hao walijifungia na wachezaji na benchi la ufundi kwa saa moja wakiteta mambo mbalimbali kuhusu mechi hiyo dhidi ya Lipuli kisha ndipo mkwanja ukatolewa kama motisha kwao ili kuimaliza kwao ili izidi kujikita kileleni inakoongoza kwa sasa na alama 67 baada ya mechi 27, ilihali Lipuli ina pointi 41 kwa michezo 30.

Advertisement