Tshishimbi apewa Sh70 milioni na sharti zito

Muktasari:

Klabu hiyo juzi ilikutana na mchezaji huyo na kumwambia apokee mzigo huo na aanguke miaka miwili, lakini yeye amesusa na kuliambia Mwanaspoti kwamba hakijaeleweka.

YANGA na kiungo wao, Papy Kabamba Tshishimbi bado wanavutaka kuhusu mkataba mpya huku wakimuekea mezani Sh70milioni zenye masharti magumu.

Klabu hiyo juzi ilikutana na mchezaji huyo na kumwambia apokee mzigo huo na aanguke miaka miwili, lakini yeye amesusa na kuliambia Mwanaspoti kwamba hakijaeleweka.

Tshishimbi anayehusishwa kujiunga na Simba, ameichezea Yanga kwa misimu miwili kuanzia mwaka 2018 akitokea Mbabane Swallows ya Eswatini zamani Swaziland.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema Tshishimbi anataka kusaini mkataba wa mwaka mmoja (ndani ya msimu mmoja) na kulipwa dola za Marekani 30,000 (sh70 millioni) kwa kucheza mwaka mmoja huku uongozi ukimwekea kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kumsajili kwa miaka miwili.

Chanzo hicho cha kuaminika ndani ya Yanga kimesema Tshishimbi, ambaye mkataba wake unamalizika mwezi ujao juzi alikutana na uongozi wakamsisitiza hilo lakini naye aliwaambia mahitaji yake.

“Msisitizo ni kusaini mkataba wa miaka miwili kwa dola 30,000 na si vinginevyo, yeye anataka asaini kwa kiasi hicho hicho kwa msimu mmoja au tuongeze hela, jambo ambao sisi hatuwezi,” kilisema chanzo chetu.

Alisema uongozi wa Yanga kwa sasa umeweka msimamo katika masuala ya usajili wa wachezaji wapya ili kujenga timu imara msimu ujao. Moja ya msimamo huo ni kusajili wachezaji ambao, wataleta matokeo na wenye viwango vya juu na ambao watadumu katika kikosi si chini ya misimu miwili.

“Tunataka kujenga timu yenye uwezo wa kuleta matokeo mazuri katika kila mechi, tumepata funzo kubwa sana msimu huu na lazima tuwe makini katika usajili,” alisema.

Kwa upande wake, Tshishimbi ambaye ana kolamu kwenye Mwanaspoti kila Alhamisi, alikiri hajasaini mkataba mpya na Yanga na wapo katika mazungumzo kwa sasa kuhusu maslahi.

“Nimewaambia nini nataka katika mkataba wangu, sasa nisuala la uongozi kuamua kama niendelee kucheza au nijiunge na timu nyingine, maana mpira ndiyo kazi yangu,” alisema.