Tshishimbi, Morrison wayeyuka, Yanga ikitua Kanda ya Ziwa

Muktasari:

Wawili hao wameshindwa kuwemo katika msafara huo kwa kile kilichosemwa na kocha Luc Eymael kuwa wana matatizo binafsi ambayo hata hivyo hakuweza kuyaweka wazi

Mwanza. Wakati Yanga ikitua Mwanza leo Alasiri tayari kwa mechi zake mbili za Kanda ya Ziwa dhidi ya Biashara United na Kagera Sugar, wachezaji Papy Tshishimbi na Bernard Morrison wamekosekana katika msafara huo.

Wawili hao wameshindwa kuwemo katika msafara huo kwa kile kilichosemwa na kocha Luc Eymael kuwa wana matatizo binafsi ambayo hata hivyo hakuweza kuyaweka wazi.

"Maandalizi yako vizuri na tunatarajia ushindi japo kuwa tunaelewa haitakuwa rahisi kwa sababu wapinzani ni wazuri na wapo uwanja wao wa nyumbani, Morison na Tshishimbi hawatakuwapo" amesema Eymael.

Kocha  Eymael amesema mchezo huo wa kwanza Jumapili dhidi ya Biashara United utakaochezwa kwenye Uwanja wa Karume Musoma,  utakuwa mgumu, lakini kwa maandalizi waliyonayo anaamini watashinda.

Yanga ambao wametoka kushinda mchezo wao wa Kombe la Shirikisho (ASFC) kwa mabao 2-1 dhidi ya  Kagera Sugar wanaenda mjini Musoma wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu uliozikutanisha timu hizo  msimu uliopita jambo linalotoa taswira ya ushindani kwa mchezo huo wa Jumapili.

Mbali na Biashara United, Kocha huyo hakusita kuitaja Kagera Sugar ambayo watacheza nayo mechi ya pili kuwa moja ya timu iliyowapa upinzani tangu ametua nchini Tanzania na kuweka wazi kuwa ni moja ya Klabu yenye ushindani mkali katika soka.

Yanga na Kagera Sugar msimu huu zimekutana mara mbili ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na nyingine ni katika mechi ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam juzi Jumanne.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Yanga ilifungwa mabao 3-0 na Kagera Sugar lakini katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Baada ya kutua Mwanza na kupokelewa na mashabiki wachache, kikosi hicho kitaunganisha moja moja kuelekea mkoani Mara kujiandaa na mtanange huo, kikihitaji ushindi ili kuendelea kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.