Tshishimbi: Mambo sita sitayasahau Tanzania

Wiki hii nitaondoka nchini nikirejea nyumbani kwa mapumziko mafupi. Ni muda sasa sijaiona familia yangu tangu kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu Bara ambao umekwishamalizika.

Nashukuru Mungu na mlipuko mzima wa ugonjwa wa Covid -19, lakini familia yangu na hata watu wangu hapa Tanzania wako salama.

Kuondoka kwangu Tanzania nimeona nisiwaache hivihivi. Acha leo niwape mambo saba ambayo katika maisha yangu ndani ya nchi hii yatabaki kuwa kumbukumbu muhimu ya kucheza soka kwa miaka mitatu.

Kwanza nakumbuka mapokezi ya mchezo wangu wa kwanza hapa nchini. Nakumbuka nilipofika mchezo wa kwanza ulikuwa dhidi ya Simba na ni mechi ya Ngao ya Hisani. Hii ilikuwa ni mechi ngumu kwangu, sikuwahi kuwa mwoga wa mechi kubwa lakini nashukuru kocha wa wakati huo, George Lwandamina alinipa maelekezo mazuri ambayo yaliniongoza kuwa bora kwa kuonyesha uwezo katika mchezo ule.

Nilichofurahi nilicheza kwa uwezo wangu, lakini mashabiki wengi waliupokea uwezo wangu vizuri na kukubali kile ambacho nilikionyesha katika mchezo. Ilinipa faraja sana jinsi ambavyo mashabiki walinipokea na nilivyofurahia haraka maisha ya kuishi Tanzania.

Pili, ni juu ya mashabiki. Unajua mchezaji yeyote ambaye hajawahi kufika nchi hii au hata kufuatilia kipi kinaendelea akiambiwa unatakiwa Tanzania, basi anaweza kuona kama anatakiwa kwenda nchi ambayo watu hawapendi soka.

Mimi nilikuwa mmoja wao, lakini nilipofika nilipata elimu tofauti. Hapa watu wanapenda sana mpira, bahati mbaya tu mafanikio makubwa yamekuwa madogo. Watanzania wengi wanapenda mpira na hili utalijua hata katika mechi ndogo na kubwa, pia kwa klabu hata timu ya taifa watu wakipoteza mechi wanaumia na wanaposhinda wanafurahi.

Watu wa hapa ni waungwana sana kama unafanya vizuri, lakini changamoto yao ni kwamba wakichukia kwa kukosa wanachotaka hubadilika na kusahau yote mazuri ambayo ulifanya. Kuna haja ya klabu na hata nchi kutumia wingi wa mashabiki katika kuendeleza mchezo wa soka hapa nchini.

Tatu, ni kukosa mataji. Hili ni baya sana kwangu, linaniumiza kila ninapofikiria kuondoka Tanzania. Iko hivi sijawahi kucheza misimu mitatu bila kukosa taji lolote, lakini sasa limenikuta hapa Yanga. Kutokana na changamoto mbalimbali za timu tumeshindwa kupata taji lolote hapa, haijawahi kunitokea kabisa tangu nianze kucheza soka la kulipwa. Nalazimika kuelewa kutokana na hali halisi ya ushindani na hata timu yetu ilivyokuwa.

Jambo la nne ni rekodi ya majeraha. Hili nalo linaingia katika kumbukumbu zangu muhimu ndani ya maisha yangu hapa Tanzania.

Hapa ndipo sehemu pekee ambayo nimekuwapo lakini siwezi kumaliza msimu bila ya kuwa majeruhi. Ukiwa mchezaji mwepesi ni rahisi kuweza hata kutamani kuondoka, lakini nilifanikiwa kuwa mchezaji jasiri kwa kuhakikisha nakabiliana na hilo na kuwa na mwenendo mzuri katika kazi yangu.

Hali ngumu ya klabu ni kitu cha tano ambacho sitaweza kukisahau hapa Yanga.

Kuna wakati hali mbaya ya kiuchumi na matatizo mengi ilipita - kulikuwa ni kipindi kigumu ambacho kama unakuwa ni mchezaji mwepesi ambaye hujakomaa unaweza kusitisha maisha yako ya kuishi hapa.

Nilikuwa mvumilivu, nilikubaliana na yote kuhakikisha nafanya kazi yangu. Wapo wachezaji ambao waliona vibaya kwa kuvumilia kwangu, lakini sikujali hilo. Niliendelea kupambana na sikuwahi kugoma kama ambavyo wengine walifanya na hata baadhi yao kuamua kuvunja mikataba.

Muhimu ni kwamba kuanzia msimu uliomalizika maisha bora yameanza kurejea Yanga angalau wachezaji wameanza kuishi maisha ambayo walikuwa wanatamani kuishi kutokana na nguvu ya wadhamini waliopo.

Jambo la sita linaloingia katika kumbukumbu zangu ni pale tulipofuzu Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, na nakumbuka hilo lilikamilika tukiwa kule Ethiopia tukicheza dhidi ya Welayta Dicha.

Nakumbuka vizuri baada ya matokeo ya hapa nyumbani tulihitaji kulinda ushindi au tusifungwe zaidi ya bao moja, na wakati huo kocha Lwandamina alikuwa ametuacha.

Tulipofika kule tuligundua kwamba mchezo ulikuwa mgumu na wenyeji wetu walikuwa wamejiandaa vilivyo, lakini pia hata ndani ya mchezo tulicheza katika mazingira magumu na bahati mbaya tulipoteza kwa bao 1-0, lakini hata hivyo matokeo hayo yalituvusha na kutinga hatua ya makundi.

Nakumbuka sikufanikiwa kumaliza mechi ile, wale jamaa walitamani kitu kwa kucheza vibaya na hatua mbaya waamuzi hawakuona haja ya kusimamia sheria, hakika ilikuwa mechi ngumu sana.

Saba na mwisho ni kwamba nilimaliza maisha yangu ya soka hapa Tanzania nikicheza mechi ya mwisho dhidi ya Simba. Si unakumbuka nilianza na Simba. Basi tambua pia mchezo wangu wa mwisho ukawa dhidi ya timu hiyohiyo.

Kinachoniumiza mechi hiyo ilimalizika vibaya kwa kupoteza kwa mabao 4-1 na hata mechi ilivyoisha maisha hayakuwa mazuri kutokana na lawama mbalimbali lakini ndio soka lilivyo. Haya ndio mambo saba ambayo sitayasahau kwa urahisi katika maisha yangu hapa Tanzania, lakini yote mema nitakuwa bado mpenzi mkubwa wa maisha ya Bongo.