Tshishimbi: Kwaherini mashabiki wa Yanga ahsanteni kwa kumbukumbu

Thursday August 6 2020

 

By PAPY TSHISHIMBI

Kuna uwezekano mkubwa huu ukawa msimu wangu wa mwishio ndani ya klabu ya Yanga. Nimeishi ndani ya klabu hii kwa miaka mitatu mfululizo tangu niliposajiliwa nikitokea Eswatini katika klabu yangu ya zamani ya Mbambane Swallows.

Tangu nilipotua hapa siku ya kwanza nikifika kukiwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba sikuwahi kujuta kuichagua hii klabu na kukubali ofa yao ya kwanza kutokana na aina ya mashabiki ambao walinipokea na nikaishi nao katika miaka mitatu hapa Tanzania.

Hii ni nchi moja nzuri na sikuwahi kuona shida na nakumbuka hata akili yangu iliwahi kufikiria kutamani hata kuwa raia na niichezee timu ya taifa hili kutokana na jinsi nilivyovutiwa na maisha ya nchi hii.

Sasa maisha yamebadilika kidogo klabu imeamua na imeshatangaza kwamba huu utakuwa msimu wangu wa mwisho kuichezea. Siwezi kupambana na wakati naona maisha yangu hapa yamefikia mwisho.

Hatua nzuri ni kwamba sikuwahi kuwa mchezaji ambaye hana mchango katika timu hii, sikuwahi kukaa nje kwa kuonekana sina kitu cha kuisaidia timu. Siku zote nimekuwa nikipambana kuhakikisha heshima ya Yanga ndani na hata nje ya uwanja inakuwa kubwa. Jambo zuri zaidi baadaye nilikuja kupewa heshima kubwa ya kuwa nahodha mkuu ndani ya klabu hii na niliyachukua majukumu hayo kwa uzito mkubwa nikipendekezwa na wachezaji wenzangu na hata makocha na uongozi kubariki.

Kumbukumbu moja mbaya itakayoniumiza ni kwamba tangu nifike Yanga sikuwahi kupata taji la Ligi Kuu Bara. Hiki ni kitu ambacho kinauumiza moyo wangu na nafikiri Yanga inakuwa klabu ya pili kuwa na historia hii.

Advertisement

Nilitamani kuacha alama katika maisha yangu kwa kupata taji nikiwa hapa, lakini kutokana na changamoto mbalimbali hili limekuwa gumu kutimia nami kuwa sehemu ya historia hiyo.

Binafsi naona hili linawezekana limechangiwa na tangu nimefika hapa kumekuwa na maisha ya milima na mabonde, na muda mrefu tumekuwa tukitengeneza timu. Mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi na hata makocha inawezekana yalichangia kuondoa ndoto ya kuwa na taji lolote la hapa ndani, lakini pia yapo ambayo tulifanikiwa kama kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kule Ethiopia.

Tumeshindwa kukubaliana na viongozi wa klabu juu ya mkataba wangu. Siwezi kusema kwamba siwezi kuja kuongeza mkataba kwa kuwa hakuna baya tulilofanyiana kati yangu na uongozi, lakini kwa sasa nafasi inayobaki ni kwamba tumeshindwa kukubaliana tofauti na tulivyoanza mazungumzo na wadhamini wa klabu.

Niliwapa heshima kubwa klabu, nilikuwa na ofa nyingi za hapa ndani, lakini niliona heshima ya kwanza kuipa klabu yangu. Zile hazikuwa ofa za kuweza kukataliwa na mchezaji ambaye hana heshima kwa Yanga. Niliwaomba waniache kwanza nijue hatima yangu na Yanga, lakini baadaye mambo hayakuwa hivyo, nilihakikishiwa nitasaini mkataba na mwisho yakatokea ya kutokea kwa klabu kunibadilikia.

Hili lilininyima raha kutokana na kila kitu kinatokea kwa wakati. Zile klabu ziliachana na mimi baada ya kuona akili yangu ipo Yanga, ambao nao baadaye yaani sasa wananiambia hawataweza kukubaliana nami na wanatangaza kuniacha.

Maisha lazima yaendelee kwa Yanga kuendelea, na mimi pia kuendelea na maisha. Muhimu niwashukuru wanachama, mashabiki na hata uongozi kwa kunipa nafasi ya kufanya kazi ndani ya hii klabu kongwe hapa Afrika.

Imani yangu ni kwamba, kutokana na mimi kuwa ni binadamu wapo ambao niliwakosea wakati nikiwa Yanga, basi nichukue nafasi hii kuwaomba radhi, lakini pia kama wapo ambao walinikosea nilishawasemehe.

Kwa sasa narudi nyumbani kwanza kutuliza akili nikitafuta akili mpya ya wapi nitacheza. Bado nina ubora mkubwa wa kucheza kwa muda mrefu. niwatakie kila la heri na mbaki salama.

Maisha ya Papy Tshishimbi kwa sasa yatabakia na mwisho ni huu ndani ya Yanga.

Advertisement