Tshishimbi : Yanga ubingwa inafeli hapa tu

Muktasari:

  • Kiungo huyo wa Yanga raia wa DRC, anafunguka kila kitu kuhusu maisha yake katika mahojiano haya maalumu na Mwanaspoti.

MASHABIKI wanaomuona Papy Kabamba Tshishimbi kafulia, hana jipya tena au kalivamia vibaya jiji la starehe la Dar es Salaam, basi majibu haya hapa.

Kiungo huyo wa Yanga raia wa DRC, anafunguka kila kitu kuhusu maisha yake katika mahojiano haya maalumu na Mwanaspoti.

SIMBA, YANGA ZINAPOFELI

Yanga na Simba ni miongoni mwa timu kongwe zaidi nchini barani Afrika tangu zilipoasisiwa 1935 na 1936. Zimekuwa zikitawala soka la Tanzania, Yanga wakiwa mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Bara wakilibeba taji hilo mara 27 na Simba ikilitwaa mara 19.

Lakini mafanikio hayo yameishia ndani tu ya mipaka ya Tanzania. Hawajawahi kutawala Afrika ukilinganisha na umri wa klabu hizo.

Yanga ilishacheza robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1969 na 1970 na Simba ndiyo timu iliyofika mbali zaidi katika michuano hiyo baada ya kucheza nusu-fainali 1974 na kutolewa na Mehalla El Kubra na wiki mbili zilizopita walitolewa katika robo-fainali dhidi ya TP Mazembe. Hamna katika ya timu hizo ambayo imewahi kutwaa taji la Afrika licha ya Simba kufika fainali ya Kombe la CAF 1993.

Tshishimbi anajua moja ya sababu zinazozifelisha timu hizo Afrika hata kama zitaendelea kutwaa ubingwa wa Tanzania.

Kiungo huyo Mcongo anasema timu hizo zinafeli kwa mambo kadhaa lakini moja kubwa ni kufanya mazoezi mara moja kwa siku.

Anasema kama kuna vitu hajavielewa kwa klabu za Simba na Yanga ni namna ya uendeshwaji wake angali anaziona zina mtaji mkubwa wa watu.

Anasema jambo la kwanza ni kuona timu hizo zinafanya mazoezi kwa siku mara moja kitu alichokiona cha ajabu kweli kweli na kinachomstajabisha ni sababu zinazotajwa kuwa ni umaskini.

“Unajua ni utaratibu mbovu sana nilioukuta huku. Kwanza nilivyoona mazoezi ni mara moja kwa siku, nilijaribu kumuuliza aliyekuwa kocha wa klabu hii, George Lwandamina, alichonijibu kilinisikitisha sana.

“Aliniambia kuwa wachezaji wanalalamika wanatoka mbali pia ishu ya nauli ni kikwazo kwao. Nikastaajabu na kujiuliza kuwa pamoja na klabu hizi kuwa maarufu na kuwa na mitaji mikubwa ya mashabiki zinashindwa vipi kupata wadhamini hata wa kuzisaidia mafuta ya kuendea mazoezini?

“Na hii ni sababu ya klabu nyingi za upande huu wa Afrika kushindwa kufanya vizuri. Hili viongozi wanatakiwa kulipa kipaumbele kwa kutafuta wadhamini. Achana na wadhamini wa ligi. Hawa wanakuwa wadhamini maalumu wa klabu kwaajili ya mazoezi ambao watawapa wachezaji hata posho za mazoezini kwaajili ya nauli na wengine walio na magari wanakuwa na vituo maalum vya kujazia mafuta ambako watakuwa wakijaza kulingana na maafikiano ya mkataba wa udhamini ambao utasaidia kuvitangaza vituo hivyo,” anasema.

Tshishimbi anatambua kuwa ili kutambia kimataifa, timu zetu zinapaswa kujiongeza katika uendeshwaji wao, zikiwamo ratiba za mazoezi.

Kiungo huyo aliongeza kuwa motisha kwa wachezaji hasa katika mazoezi zinawaongezea morali ya kupambana kwaajili ya kuhakikisha wanapambania vitu vitatu; posho, pointi tatu na kuifanya timu kuwa bora na ya ushindani kitu ambacho kwa hapa hajakiona na kimekuwa kikichangia wachezaji kuwa wavivu kufanya mazoezi.

KUMBE NI MJESHI

Katika maisha ya kawaida kila mwanadamu anakuwa na ndoto na malengo yake tangu akiwa na umri mdogo kuwa akikuwa anatamani kuwa nani? Au anatamani kumiliki nini basi Mwanaspoti linataka kukujuza ndoto za kiungo wa Yanga Tshishimbi.

Anasema alivyokuwa ana umri mdogo pamoja na kucheza sana mpira lakini ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuwa mwanajeshi lakini ndoto yake ilivunjwa na mzazi wake ambaye hakutaka kabisa kusikia mwanae anaingia huko.

“Nilikuwa muumini wa michezo ya ngumi na karate. Nilikuwa nacheza sana na kufuatilia michezo hiyo huwezi kuamini nilishapata hadi nafasi ya kujiunga na jeshi lakini cha kushangaza baba yangu mzazi alikuja na kunichomoa.

“Hadi leo hii ukiniuliza ni kwanini baba yangu alikatisha ndoto yangu siwezi kukwambia sababu kwani sijaijua. Sielewi aliona nini kwangu hadi kuamua kuchukua uamuzi huo, hivyo ndoto yangu ya uanajeshi ilikatishwa kwa namna hiyo na nimejikuta nimeibukia huku kwenye soka japo pia kilikuwa ni kitu nilochokuwa nakipenda,” anasema.

NI WAKALA

Tshishimbi pamoja na kuwa ni mchezaji lakini amefanikiwa kuwa na jicho la kuona vipaji vya wachezaji na ndiyo maana alifanikiwa kumleta straika Mcongo mwenzake, Heritier Makambo, Yanga.

“Mimi ni wakala lakini bado sijaanza kunufaika kwasasa nafanya kama msaada kwa vipaji vya wachezaji wenzangu na tayari nimeshafanya kwa baadhi ya wachezaji ambao wana mafanikio kwenye klabu nilizowapeleka.

“Si Makambo tu pia kuna Fiston Kayembe ‘Festo’ ambaye pia nilimtafutia nafasi Yanga lakini alikwama kutokana na kukosa vibali nikaamua kumpeleka Zesco ambako anafanya vizuri zaidi na anatamani kurudi Tanzania kuja kucheza.

“Hao ndiyo baadhi ya wachezaji wenye mafanikio ambao nimewatafutia timu. Hiki ndiyo kitu kingine kinachonibeba na kunifanya hata nikistaafu soka nifikirie kuwa wakala wa wachezaji ni kuaminiwa na makocha ambao wamekuwa wakinitumia kutafuta wachezaji,” anasema.

“Napenda kucheza soka sitamani kustaafu mapema lakini ikitokea nikastaafu kutokana na umri basi nitakuwa na ajira yangu binafsi ya kuwatafutia wachezaji timu. Sitakuwa na kazi ngumu kufanya hivyo kwani tayari najua kuona kipaji cha mchezaji na naaminika na baadhi ya makocha,” anasema.

ANAHUSUDU RASTA

Kila mchezaji ana staili yake katika uchezaji, muonekano na hata namna ya kuishi. Kwa Tshishimbi humwambii kitu kuhusu rasta.

Kama unadhani rasta zake alianza kuzitengeneza akiwa ameshapata umaarufu basi unajidanganya. Kiungo huyo ni muumini wa nywele kichwani kwake tangu anaanza kucheza soka akiwa na umri mdogo.

“Napenda kuwa na nywele kichwani na sijui kama naweza kucheza bila ya kuwa na nywele kichwani, nimeshazoea sijaanza hivi karibuni. Tangu nina umri mdogo nilikuwa na rasta kichwani ila ninachobadili ni staili tu,” anasema.

“Sijashawishiwa na mtu ni mapenzi yangu mwenywe ningekuwa nimeanza ukubwani basi ningekuwa na sababu au na mtu aliyenifanya niwe hivi, lakini nahisi imetokea tu nimeamua kuwa hivi.”

Basi nakudokeza kuwa usione anapendeza kichwani kwake ukajua anatengeneza kwa bei rahisi. Mafundi zake wanaingiza kipato kupitia yeye kwani akienda kuosha na kuzitengeneza anatumia Sh. 50,000 ambazo anaweza kukaa nazo wiki mbili au tatu anarudi tena kutengeneza.

“Gharama ya kutengeneza inategemea kwani zikichafuka sana bei inakuwa kubwa ambayo ndiyo hiyo Sh.50,000. Zikiwa hazijachafuka sana huwa nafanyiwa Sh.20,000 na kazi yangu hii ya kucheza siwezi kukaa muda mrefu bila kuosha kwani hazipatani na joto, zinawasha,” anasema.

AMKUMBUKA ROSTAND

Najua hujui na mimi nataka kukujuza zaidi. Unaambiwa Tshishimbi ambaye huu ni msimu wake wa pili kukipiga katika klabu ya Yanga, alikuwa ni rafiki mkubwa wa kipa Youth Rostand ambaye alitupiwa vilago na matajiri wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kufanya vizuri.

Anasema alipofika katika klabu hiyo Rostand ndiye rafiki yake wa kwanza aliyempokea vizuri na walikuwa wanaishi vizuri na aliumia sana alipotupiwa virago.

“Namkumbuka sana na naumia sana kumuona anakaa nyumbani bila kazi kwani tangu ametupiwa virago na Yanga hadi sasa bado hajapata timu. Naumia sana kwani naamini ana uwezo mkubwa aliouthibitisha akiwa African Lyon kabla ya kutua Yanga.

“Kutimuliwa kwake Yanga haiwezi kuwa sababu ya mimi kuacha kuendeleza mawasiliano na mtu ambaye niliishi naye vizuri. Bado tunawasiliana na kaniambia hana timu. Hicho kitu kinaniumiza sana,” anasema Tshishimbi.

Usikose sehemu ya pili kesho Ijumaa uone mambo ya giza yaliyomtokea Yanga.