Tshabalala, Kagere waoga noti Taifa

Muktasari:

  • Wachezaji wa Simba. Mohammed Hussein 'Tshabalala' na Meddie Kagere wamejikuta wana maisha mazuri ndani ya kikosi hicho baada ya kuzawadiwa pesa na mashabiki wa timu hiyo kutokana na kufanya kwao vizuri katika mechi zilizopita.

NAHODHA Msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na straika kinara wa mabao wa klabu hiyo katika Ligi Kuu msimu huu, Meddie Kagere wamefanyiwa sapraizi kwa kumwagiwa noti wakitoka kuisaidia timu yao kuinyuka African Lyon kwa mabao 2-1.

Simba ikicheza bila ya aliyekuwa Kocha Msaidizi wao, Masoud Djuma, ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Taifa na kuifanya ifikie alama 14 na kupanda hadi nafasi ya nne (kabla ya mechi za jana Jumapili), lakini furaha zaidi iliongeza kwa kina Kagere na Tshabalala.

Hii ni kwa sababu mara baada ya mchezo huo uliopigwa usiku, nyota hao walizawadiwa fedha na kundi al wanachama wa klabu hiyo waitwao, Simba Kwanza kila mmoja akivuta Sh 150,000 kama kuwapa motisha zaidi kwa kazi wanayofanya Msimbazi.

Tshabalala ndiye alikuwa wa kwanza kukabidhiwa pesa hizo ambapo walimpa risala fupi wakimweleza wanatambua msimu uliopita alisumbuliwa na majeraha na kwamba kwa sasa yupo fiti hivyo aendelee kuwapa raha Wana Msimbazi walio nyuma yao. Tshabalala, alilidokeza Mwanaspoti baadaye kuwa, zawadi aliyopewa kwake ni kama deni alilikopeshwa na wanachama hao na anapaswa kulipa deni hilo uwanjani. “Ni faraja kubwa kwani tupo wachezaji wengi lakini bahati leo imeangukia kwangu, hili ni deni napaswa kupambana ili nitimize wanachokitaka kwangu. “Ni kiu ya kila mchezaji kuhakikisha anaonyesha kiwango cha juu ili kutetea ubingwa wetu huu,” alisema.