TryAgain: Hii ni Simba nyengine kila idara ni moto

JULAI 2, 2017, Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Simba, iliwateua wajumbe wa kamati hiyo, Abdallah Salim na Iddy Kajuna kuwa wasimamizi wa majukumu ya Simba.

Hatua hiyo ni baada ya Rais Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kushikiliwa na vyombo vya dola kwa sababu mbalimbali.

Salim maarufu kama Try Again anakaimu nafasi hadi hapo uchaguzi utakapofanyika kuchagua viongozi watakaoisimamia Simba kwa miaka mingine minne kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.

Katika kuadhimisha Simba Day 2018, Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu na TryAgain kuzungumzia masuala mbalimbali ya klabu.

Salim alianza kwa kuwashukuru watu wote hasa wanachama kwa kuwaamini na kuwapa jukumu zito la kuiongoza Simba.

“Niseme kwa kifupi tu kwamba tumefanikiwa katika maeneo mbalimbali tangu tuichukue Simba na sasa mabingwa kama mnavyoona.Wakati tunaichukua Simba, ninakumbuka ilikuwa kipindi cha usajili, tulihangaika kuitengeneza Simba, tumefanya usajili wa wachezaji tunaoamini watatusaidia na kuipa Simba mafanikio na sasa mabingwa.

“Yako mengi ya mafanikio kwa kweli, tumefanya tamasha la Simba Day mwaka jana na leo hii tuna tamasha lingine Agosti 8 (leo Jumatano).

“Lile lilikuwa tukio la aina yake kutambulisha wachezaji wetu lakini mwaka huu litakuwa bora zaidi. Tulifanya mkutano wa wananchama wa kujitambulisha lakini pia kuwaomba baraka zao kuelekea Ligi Kuu, tumefanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala na hii ni ya wanachama na mafanikio haya ni kwa ajili yao.

“Tulicheza Ngao ya Jamii, tuliifunga Yanga na tumeona ligi inamalizika na Simba inatwaa ubingwa na mechi mkononi, lakini raha zaidi kumfunga mtani.

“Yako mengi, mengi...tumefanya mabadiliko benchi la ufundi, tumebadilisha walimu sasa Simba inanolewa na Patrick Aussems na Masoud Djuma. Ilishtua mashabiki na wapenzi wa soka kumwondoa Joseph Omog na Jackson Mayanja wakati ule, tukamleta Pierre Lechantre lakini yote ni katika kuweka sawa. Kuna mengi ya mafanikio Msimbazi.”

Mahojiano na Try Again yalikuwa hivi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Simba Day

Swali: Nini hasa mmekiandaa katika Simba Day?

TryAgain: Kama nilivyosema awali, mwaka huu tumeandaa mambo mbalimbali. Mambo ni mengi zaidi ya kutambulisha wachezaji na jezi, tutafanya shughuli mbalimbali kuadhimisha siku hii.

Kuna wanaotembelea wagonjwa, kufanya usafi, tunashirikisha matawi katika maeneo mbalimbali na hata siku hii, tutaanza mapema uwanjani, mechi za vijana na timu yetu ya wanawake, atakayekuja uwanjani ataburudika na ataiona kweli Simba iko kimkakati zaidi.

Swali: Lakini mara zote timu ya Simba imekuwa ikifanya vibaya siku hii. Kwanini?

TryAgain: Ni kweli, inawezekana wachezaji hawajazoeana lakini mwaka huu au msimu huu si Simba ile iliyozoeleka, kwani tumejipanga na kama mnavyoona timu ilikuwa Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya ligi.

Swali: Umezungumzia kambi ya Simba Uturuki, lakini kuna huyu mchezaji wenu, Haruna Niyonzima hayuko na wenzake Uturuki, suala lake likoje?

TryAgain: Haruna aliomba ruhusa kwenda kwao na alijua kuwa atachelewa kurudi ndio maana akaagiza akatiwe viza yake ya Uturuki, sasa tarehe ambayo alitakiwa kurudi ilikuwa ni Julai 20 na kama ilivyokuwa mwaka jana alikosa pre-season hata kiwango chake hakikuwa kizuri kwa sababu ya kukosa ‘pre-season’ na kukaa pamoja na wenzake.

Upo utaratibu na namna ya kufanya, kama ni makosa basi tutamwadhibu kwa mujibu wa utaratibu wetu lakini tutampa nafasi ya kujieleza kwa nini hajajiunga na timu.

Swali: Hebu tueleze, watu wanataka kuijua Simba hii, nini kitarajiwe msimu ujao?

TryAgain: Hii ni Simba nyingine kabisa. Tumejipanga, kama nilivyosema tuko kimkakati zaidi. Tumefanya usajili mkubwa na zaidi tunalenga kufika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hatutaki kuwa Simba ya kufikiria timu sijui wanakuja Waarabu…au TP Mazembe, sisi tumejipanga kwa kila eneo.

Usajili wetu tumechanganya, kuna vijana, umri wa kati na hii ni kwamba hatutaki kupata tabu sana. Kikosi cha msimu uliopita, tulitwaa ubingwa, lakini tulipata tabu sana, hatukuwa na kikosi kipana, safari hii tumekamilika kwelikweli.

Swali: Kwa hiyo unataka kusema msimu ujao hamna shaka nao kwa jinsi mlivyojipanga?

TryAgain: (Anatabasamu) Hilo liko wazi, kwa Simba hii nani wa kuizuia? Wasiwasi wetu inaweza kuwa ligi ya timu chache. Tunataka ligi iwe ya ushindani kwa timu zote kwani hapo ndipo utaona thamani yenu kuliko kuwa na timu nyingi lakini dhaifu. Timu zitakazokutana na sisi ukweli zijipange hasa.

Swali: Kuanzia Desemba mwaka huu, mtakuwa na ratiba ngumu mechi za CAF, Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi, FA Cup mnajipanga vipi?

TryAgain: Kazi kubwa ni hii ya kusajili. Msimu ujao tunafahamu tuna ratiba ngumu. Tuna mashindano sita na ndiyo maana tumesajili kwa malengo. Kama mlivyoona tumepeleka timu tofauti katika mashindano ya SportPesa na Kombe la Kagame, yote ni kuangalia viwango na bahati nzuri wamefanya vizuri, timu imecheza fainali japokuwa hatukufanikiwa kutwaa ubingwa. Tumejipanga kwani hilo tumeliona na hatuna shaka na kikosi chetu kwani ni kikosi kipana.

Swali: Kuna watu wanawasajili wa chezaji kisha wanawaambia wacheze chini ya kiwango hilo likoje?

TryAgain: Unajua ukiwa kiongozi, lazima ujue matatizo ya wachezaji. Hapa ni suala la nidhamu na performance (kiwango), wachezaji hata kama kasajiliwa na nani, afahamu yeye ni mali ya klabu. Tunakaa nao na tumewaambia kuwa kama kuna matatizo, kuna njia za kuyafikisha, suala la kiufundi kuna kocha, kama ugonjwa yupo daktari kama kuna shida nyingine, tumeanzisha email (barua pepe) kwa wachezaji za kuwasiliana kama kuna tatizo, lakini si kucheza chini ya kiwango kumbe una yako.

Swali: Katika Simba Day mtazindua jezi mpya, mna mkakati gani wa kuifanya jezi kuwa kizalishi cha fedha?

TryAgain: Hili ni tatizo sugu. Tutafungua duka klabuni halafu tutawapa mawakala maalumu wa kutuuzia jezi zetu. Tatizo wachapishaji ni wengi, wakiiona aina tu, tayari kesho iko barabarani kwa ubora hafifu. Tutatoa maelekezo kwa anayetaka jezi ya Simba halisi ataipata wapi pamoja na bei. Simba inapanga kuuza jezi 40,000.

Tutaanzia hapa. Lakini pia niweke sawa hapa, Simba inatumia rangi mbili, nyekundu na nyeupe, lakini niseme tu inawezekana kutumia pia rangi nyingine, iko kikatiba. Mfano; ikitokea mdhamini anakuja na bluu basi Simba itabidi iwe hivyo na uzuri iko kikatiba.

Swali: Suala la uwanja wa klabu likoje?

TryAgain: Hili ndilo linatuumiza vichwa. Makocha hawataki kusikia viwanja visivyo na ubora na ukiangalia kwa sababu, vinasababisha majeraha kwa wachezaji. Lakini niseme tu, mwezi huu haumaliziki Simba itakuwa na pa kuanzia kuhusu uwanja.

Unajua tumekwama kwa kuwa kuna suala la kesi ambalo liko mahakamani lakini mwelekeo upo na mwezi huu wa nane haumaliziki, tukimaliza Simba Day tunakwenda Bunju kuanza mkakati wa uwanja kwani kukodi uwanja ni gharama kubwa.

Swali: Suala la wadhamini limekaaje Simba?

TryAgain: Kwanza niwashukuru SportPesa kwa kutuunga mkono, wadhamini wetu wengine Azam na wengine wote wanaotusapoti. Mwaka huu kuna baadhi ya mashirika na kampuni zinataka kuingia Simba, sitaki kusema moja kwa moja kwa kuwa mazungumzo bado yanaendelea.

Swali: Simba mmekuwa na kawaida ya kutimua makocha hata kama timu iko pazuri, huoni inavuruga wachezaji kwani kila mwalimu anakuja na mfumo na staili yake?

TryAgain: Ni kweli, lakini kinachoangaliwa ni kiwango (performance). Hatukatai Simba inakuwa pazuri lakini huo uzuri ni kwa kiwango? Tukiona haya mambo hayaendani, tunakaa na kuangalia jinsi ya kuboresha na zaidi ni kubadilisha benchi la ufundi. Ni mambo ya kawaida katika klabu na zaidi ni kulenga mafanikio.

Na katika kujipanga zaidi hapa, tutaajiri msoma mchezo (game analyst) ambaye atakuwa na kazi ya kusaidia benchi la ufundi. Kazi yake kubwa ni kuandaa taarifa zote zote za mpinzani, kushauri kwenye kufanya ‘sub’ na aina ya mchezo wanaotakiwa kucheza kulingana na mazingira. Huyu ataipunguzia kazi kubwa benchi la ufundi.

Swali: Ligi Kuu inakaribia kuanza, Agosti 22. Unadhani ni zipi kasoro zinazoharibu ligi?

TryAgain: Kuna changamoto nyingi. Ligi ina makandokando mengi, gharama za uendeshaji, kuna waamuzi lakini kubwa ni ratiba ya ligi. Hii panguapangua ya ratiba inachanganya sana na inavuruga mpango wa timu. Pia, unaweza kukuta ratiba inaielekeza timu moja kucheza mechi mfululizo Kanda ya Ziwa kwa mfano, inamaliza mechi zake huko wanatoka na visenti.

Ni vyema timu ikacheza na ipangiwe muda mwingine wa kurudi huko kwani kukaa nje ya kituo kwa muda mrefu ni gharama pia. Mechi mbili nje, mbili nyumbani, au wakati timu inarudi, njiani inaweza kupangiwa mechi.