Try Again kurudi Msimbazi

Saturday November 10 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

Dar es Salaam. ALIYEKUWA Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' ana asilimia kubwa ya kubaki ndani ya Simba kama mmoja ya wajumbe wanaoingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti wao Mohamed Dewji 'Mo Dewji'.
Mo Dewji ndiye aliyepita katika mchakato wa uwekezaji kwa Sh 20 bilioni akimiliki hisa asilimia 49 huku klabu ikibaki na asilimia 51 ambapo kila upande unaingiza wajumbe nane na hivyo kuwa na jumla ya wajumbe 16 wa Bodi hiyo.
Kama hujui ni kwamba leo Jumamosi, Mo Dewji atakutana na wajumbe wa Simba waliochaguliwa wiki iliyopita ili kutambulishwa kwake, huku ikielezwa Try Again akipigiwa chapuo kubakisha Msimbazi kwa kazi nzuri aliyoifanya klabuni hapio.
Katika uchaguzi huo, Swedy Mkwabi alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa upande wa Simba SC Company Limited huku wajumbe wakiwa ni Dk. Zawadi Kadunda, Hussein Kitta Mlinga, Mwina Kaduguda, Asha Baraka na Seleman Haroub.
Imeelezwa kikao cha leo kitafanyika katika ofisi za bilionea  huyo kabla ya kufuatiwa semina ya wajumbe hao ili kupigwa msasa wa mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu ambapo sasa wanaingia mfumo wa hisa.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema wadau wengi wanapendekeza Try Again awe miongoni mwa wajumbe wawili wa kuteuliwa ingawa jukumu hilo limeachwa mikononi mwa Mkwabi ambaye ndiye mwenye jukumu la uteuzi kikatiba.
"Kikao kitaanza saa 9 alasiri ofisi za Mwekezaji wetu, baada ya kikao kutakuwa na semina ya kutuelekeza mambo mbalimbali kuhusu klabu na mfumo mpya wa kampuni, maana hatuwezi kuingia na kuanza kazi moja kwa moja."
"Ni lazima tufundishwe ili tuelewe kama tukianza majukumu kila mmoja awe anafahamu nini cha kufanya. Kuhusu Try Again ni kiongozi mzuri nadhani hadi sasa anaendelea na majukumu yake ya klabu kama kawaida kwani tulioingia bado hatujui vitu vingi na kuna uwezekano mkubwa wa kuwa miongoni mwa wajumbe wa kuteuliwa na itapendeza akiwa mmoja wapo ingawa Mwenyekiti ndiye mwenye nguvu ya kuamua nani amteue," alisema Mjumbe huyo.
Kwa upande wa Mkwabi alisema bado hajateua wajumbe hao ila muda ukifika atawateua na kuwatangaza kwani ni moja ya majukumu yake ingawa alikiri kumuomba Try Again kuendelea na majukumu yake hadi hapo wajumbe wapya watakapouelewa mfumo.
"Bado kidogo, nikikamilisha nitawatangaza maana ni lazima kila kitu kikamilike, uongozi uliopita watatukabidhi nyaraka ili tuzipitie kama kuna kujadiliana baadhi ya mambo itakuwa hivyo, hivyo tusubiri tu wakati wowote," alisema Mkwabi.
Wakati wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita, Try Again ambaye hakugombea alisema yeye ni mwanachama wa Simba, anaipenda Simba na yupo tayari kushirikiana na uongozi mpya iwe ushauri ama vyovyote.

WACHAMBUZI WANENA
Dk Mshindo Msolla aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars alisema endapo Try Again atakuwa kwenye bodi hiyo basi Wanasimba watafaidi matunda yake.
"Try Again sio mtu mwenye tamaa, Simba wana mtu sahihi wa kuwaongoza, kikubwa Mkwabi katika nafasi zake hizo mbili akimuingia Try Again watakuwa wamelamba dume, mtu huyo ni mtetezi mkubwa wa maslahi ya klabu.
"Ni mtu sahihi, kwani aliikuta Simba ikiwa kwenye mazingira magumu alisimama na kuipigania mpaka kufikia mafanikio ya ubingwa na mabadiliko haya, nilishangaa niliposikia hagombei Uenyekiti na sasa nitafurahi kama atakuwemo kwenye bodi maana ana dhamira ya kweli hana tamaa," alisema Dk Msolla.
Naye Ally Mayay alisema, "Mambo mengi awali ndani ya Simba yalikuwa yanakwama lakini alipokabidhiwa Try Again kila kitu kilikwenda vizuri, kwanini asiwekwe kwenye Bodi ya Wakurugenzi, ni mtu sahihi kabisa, bila nguvu ya Try Again sidhani kama Simba ingefikia hatua hii kubwa. Uwepo wake utasaidia kwenye mambo ya maamuzi kwani anajua biashara na anafahamu mpira, atatetea maslahi ya timu kwani hakuna biashara bila soka kua safi," alisema Mayay.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Simba SC Company Limited, Crescentus Magori, Mayay alisema; "Wanasimba wamelamba dume, Magori anajua biashara maana amekaa NSSF kwa zaidi ya miaka 10 hivyo anafahamu vyema mambo ya hisa na anapenda mpira, atawasaidia kwa kuwa ana mchango mkubwa tangu awali,".
Katika kikao hicho pia kitajadili juu ya kocha msaidizi atakayechukuwa nafasi ya Masoud Djuma ambapo awali jina la Seleman Matola ndilo lilikuwa mezani pamoja na maandalizi ya michuano ya kimataifa ambapo Simba wataanza nyumbani dhidi ya Mbabane Swarrors ya Lesotho kati ya Novemba 27 hadi 29.

Advertisement