Toto Africans kimenuka huko Mwanza!

Muktasari:

  • Kocha huyo anaachia ngazi huku akiicha timu katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Pili kwa pointi 11 nafasi ya pili kwenye kundi lao B.

Mwanza. KOCHA Mkuu wa Toto Africans,Ibrahim Mlumba ametangaza kuachia ngazi katika kikosi hicho akidai kuingiliwa majukumu na kutothaminiwa na Katibu Mkuu,Chassa Yahya aliyetuliwa kwa muda.

Mlumba ameisaidia timu hiyo kuwa nafasi ya pili kwa pointi 11 katika Ligi Daraja la Pili kwenye kundi lao B linaloongozwa na Gipco FC wenye alama 12 baada ya kushuka uwanjani mara nane.

Toto Africans ambayo iliwahi kutesa Ligi Kuu miaka ya nyuma kwa sasa haina uongozi kwani aliyekuwa Mwenyekiti wake,Godwine Aiko alitangaza kujiuzuru na sasa inaendeshwa kiaina tu.

Kocha Mlumba alisema kuwa licha ya kujituma na kuwahamasisha wachezaji kucheza bila kufikiria mazingira magumu waliyonayo,lakini amekuwa akiingiliwa majukumu na hathaminiwi na Katibu wake.

 

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo yeye hatoweza kuendelea kuifundisha timu hiyo na kwamba,tayari ameshapata taarifa kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Klabu hiyo kuandaliwa barua ya kusimamishwa.

“Sasa Katibu yeye anaingiliaje mazoezi ya timu badala ya kutafuta vyanzo vya pesa ili kukidhi mahitaji ya timu? Mimi sitaweza kuendelea kwa sababu naingiliwa majukumu na siheshimiwi”alisema Mlumba.

Kwa upande wake Katibu huyo wa muda Yahya, alikanusha vikali tuhuma hizo na kwamba bado wanaamini Mlumba ni Kocha wao isipokuwa anashangaa kutohudhuria mazoezini.

Alisema kuwa hata hivyo bado hawajajua sababu ya Kocha huyo kutokuja mazoezini na kwamba iwapo ataona dalili za kuachana na timu basi watafanya haraka kusaka mbadala wake.

“Hata leo (juzi) Mlumba hajaja mazoezini na sijui tatizo ni nini kwa sababu hatudai,bado ninaamini ni Kocha wetu lakini tukiona dalili zozote za kutuachia timu basi tutatafuta mwingine”alisema Katibu huyo.