Torreira amrudisha kazini Granit Xhaka

Muktasari:

Granit Xhaka alionekana kuchoka kwenye kikosi cha Arsenal mwishoni mwa msimu, lakini baada ya ujio wa Lucas Torreira umemfanya kiungo huyo kurudi kwenye ubora wake upya huko Emirates

STAA wa zamani wa Arsenal, Martin Keown amesema Granit Xhaka anapaswa kumshukuru sana Lucas Torreira kwa sababu ameokoa ajira yake huko kwenye kikosi cha Emirates.
Torreira ameanzishwa katika mechi tatu za mwisho za Arsenal na Keown ametazama mechi hizo na kuona Xhaka ameanza kucheza kwa ubora wake kutokana na kupangwa na mtu anayefahamu wajibu wake ndani ya uwanja na kumwaacha Mswisi huyo awe huru uwanjani.
Keown, ambaye alikuwa beki mahiri wa kati wa kikosi hicho cha Arsenal kilipokuwa chini ya Arsene Wenger alisema: “Kitu cha wazi kukiona ni kwamba wameshinda mechi tatu mfululizo za ugenini, wakati msimu uliopita walishinda mechi nne tu kwa msimu wote.
“Ukweli sikuthubutu kutazama mechi za Arsenal inapokwenda ugenini kwa msimu uliopita, lakini kwa sasa ukiwatazama unapata raha. Ukitazama ule mpira unaochezwa, hasa lile bao la Aaron Ramsey unaweza kuona Arsenal iliyotofauti kabisa.
“Lucas Torreira amekuja kuleta uwiano mzuri kwenye sehemu ya kiungo. Amemfanya Granit Xhaka kuwa huru na kufanya jambo moja la kutengeneza nafasi tu."
Arsenal kwa sasa ipo chini ya kocha wa Kihispaniola, Unai Emery ambaye mambo yake yamekuwa matata kabisa na kukifanya kikosi hicho cha Arsenal kuwa tofauti na walivyokuwa msimu uliopita na mingine huko nyuma.