Top four zitakavyopenya mtoano mabingwa Ulaya

Saturday November 9 2019

Top four -zitakavyopenya -mtoano -mabingwa -Ulaya-Olympiaco-Club Brugge-Jurgen Klopp -

 

LONDON ,ENGLAND .BAYERN Munich, Juventus na Paris Saint-Germain zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kila timu kucheza mechi nne to kwenye makundi yao na wameshinda mechi zilizopita dhidi ya Olympiacos, Lokomotiv Moscow na Club Brugge, kama zilizovyopangwa kwa kufuata mtiririko.

Vigogo hao watatu wa Ulaya wamepenya hatua ya mtoano kwa kuongoza makundi yao baada ya mechi nne tu. Sasa klabu za Ligi Kuu England zilizopo kwenye michuano hiyo, Liverpool, Man City, Tottenham na Chelsea zinamatumaini makubwa ya kuungana na Bayern, Juve na PSG katika mtoano huo wakati zitakapocheza mechi zao za tano kwenye makundi.

Hiki ndicho kinachoweza kutokea kuhusu majaliwa ya klabu za Ligi Kuu England kwenye mchakamchaka huo wa kuingia hatua ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu wakati timu zitakazocheza mechi zao za tano kwenye makundi.

Liverpool

Kwenye mchezo wao wa tano katika kundi, Liverpool watakuwa na kazi moja ya kutaka kulipa kisasi dhidi ya Napoli baada ya kupoteza mechi yao iliyopigwa Naples kwa mabao 2-0 mwezi Septemba. Liverpool ambao ni mabingwa watetezi watakuwa wamefuzu hatua ya 16 bora kama watapata ushindi kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Napoli.

Lakini, kikosi hicho cha Jurgen Klopp bado kitafuzu tu hatua ya 16 kwenye mechi hiyo ya tano hata kama itafungwa ila kama tu RB Salzburg watashindwa kuwafunga Genk.

Advertisement

Man City

Manchester City wangekuwa washafuzu hatua hiyo ya 16 bora kama wangeshinda mchezo wao uliopita dhidi ya Atalanta. Bao la Mario Pasalic lililokuwa la kusawazisha baada ya lile alilofunga Raheem Sterling kuwatanguliza Man City liliwatibulia wababe hao wa Pep Guardiola kutinga hatua hiyo ya mtoano.

Man City matumaini yao ya kutinga hatua hiyo yatakuja kwenye mechi ya tano kama watawachapa Shakhtar Donetsk na kwenye mechi iliyopita waliwachapa 3-0. Man City bado watafuzu hata kama watatoa sare au kufungwa na Shakhtar kama tu Atalanta hawatakuwa wamepoteza dhidi ya Dinamo Zagreb.

Tottenham

Ushindi mara mbili mfululizo dhidi ya Red Star Belgrade umewaweka Tottenham kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kufunga kwenye mbili za kwanza. Ushindi dhidi ya Olympiacos kwenye mchezo ujao utawafanya Spurs wawe wametinga kwenye hatua hiyo ya 16 bora na kwenye mechi ya kwanza walipoteza uongozi wao wa mabao mawili. Kikosi hicho cha Kocha Mauricio Pochettino bado kinaweza kufuzu raundi inayofuata kwa kutoka tu sare na Olympiacos, lakini kama tu Bayern Munich wataichapa Red Star Belgrade.

Chelsea

Kundi H linaonekana kuwa na upinzani mkali zaidi katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko kawaida. Vinara Chelsea na wanaoshika nafasi ya pili Ajax na wale kwenye nafasi ya tatu, wote wana pointi saba wakielekea kwenye mchezo wa tano kwenye makundi yao.

Chelsea wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Valencia, wakati Ajax wao watakuwa nyumbani kuwakaribia Lille, ambao hadi sasa wana pointi moja tu. Chelsea hiyo ya Frank Lampard itafuzu hatua ya 16 bora kama tu wataweza kuichapa Valencia kwenye mechi hiyo ya tano huku wakiomba Lille wakaze dhidi ya Ajax na kutoka nao sare tu inatosha. Hapo watakuwa wamefikisha pointi 10 na mechi ya mwisho itawakutanisha wenyewe kwa wenyewe, Ajax na Valencia.

Advertisement