Tizi la KMC hakuna kupoa

Timu ya KMC imeendelea na mazoezi leo Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama, Dar es Salaam kujiandaa na michezo ya mwisho ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu 2019/20.
Moja ya mazoezi ambayo kocha Mkuu, Haruna Hererimana alikuwa akiwapa wachezaji wake ni kupiga pasi kwa haraka pamoja na kulenga mashuti langoni.
Awali kocha aligawa timu katika makundi manne, makipa, mabeki, viungo na washambuliaji na kila moja kupewa mazoezi yake binafsi.
Hererimana alikuwa akiwaelekeza wachezaji wake kupiga pasi zisizozidi tano kisha kutoa pasi kwa haraka huku wakihakikisha hawagusani, ikiwa moja ya njia ya kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona.
"Toa mpira kisha tafuta nafasi haraka, hakikisha pasi yako inafika kwa muhusika, usitoe mpira kama huna uhakika na unayempa," alisikika Hererimana akiwaelekeza wachezaji wake.
KMC inashirika Ligi Kuu msimu wa pili ikiwa nafasi ya 15 baada ya kucheza kukusanya alama 33 katika mechi 29 ilizocheza hadi sasa
Kocha huyo aliyeanza msimu akiwa na Lipuli FC alitua kwenye kikosi cha KMC kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja aliyetimuliwa mwishoni mwa mwaka Jana kutokana na matokeo mabovu ambayo timu hiyo ilikuwa ikiyapata.
KMC iliyopanda Ligi Kuu chini ya kocha, Fredy Felix 'Minziro', msimu uliopita ilimaliza ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi baada ya kukusanya alama 40 jambo lililowawezesha kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika